Yanga SC

HAKUNA KISINGIZIO YANGA WOTE WAPO VITANI

Vardo June 4, 2026 1:42 pm

KLABU ya Yanga imeendelea na maandalizi yake kuelekea hatua za mwisho za msimu, huku ikieleza kuwa kikosi chake kiko katika hali nzuri ya afya na utimamu wa mwili kabla ya michezo iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema benchi la ufundi linaendelea kuinoa timu kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha inakuwa tayari kwa changamoto za mechi zijazo ambazo ni muhimu katika kufanikisha malengo ya klabu msimu huu.

Kamwe amesema hali ya kikosi inaridhisha kwa kuwa hakuna mchezaji anayesumbuliwa na majeraha makubwa yanayoweza kuvuruga mipango ya benchi la ufundi, jambo ambalo limeongeza morali na ushindani miongoni mwa wachezaji.

 

“Maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho. Tunashukuru kwa sasa hakuna majeruhi na wachezaji wote wako tayari kupambana kwa ajili ya kuisaidia Yanga kufikia malengo yake,” amesema Kamwe.

Amebainisha kuwa kila mchezaji anatambua uzito wa michezo iliyosalia, hivyo ari na nidhamu katika mazoezi imeongezeka huku kila mmoja akipambana kuhakikisha anakuwa sehemu ya kikosi kitakachopewa majukumu katika mechi hizo.

Yanga inatarajiwa kurejea dimbani Juni 13 itakapokuwa mgeni wa Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Mchezo huo unatajwa kuwa miongoni mwa mechi muhimu kwa mabingwa hao watetezi, ambao wanaendelea kupigania pointi muhimu katika mbio za kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, huku pia wakisaka mafanikio kwenye Kombe la Shirikisho.

PACOME AKIWA FITI, YANGA YAONGEZA KASI YA UWINDAJI WA MAKOMBE NYUMA YA YANGA KWA ALAMA MBILI, BARKER BADO ANAAMINI SIMBA KUTWAA UBINGWA