kimataifa

MAHAKAMA YA KITAIFA YAIAMURU TANZANIA KUONDOA ADHABU YA KUNYONGWA

Vardo June 6, 2026 7:14 pm

Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imeiamuru Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho katika Kanuni yake ya Adhabu na kuondoa adhabu ya kifo ya lazima kwa watu wanaopatikana na hatia ya mauaji pamoja na kuondoa kunyonga kama njia ya kutekeleza adhabu hiyo.

Uamuzi huo unaigusa moja kwa moja Kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu ya Tanzania ambacho kwa sasa kinatoa adhabu moja tu kwa kosa la mauaji, ambayo ni kifo kwa kunyongwa bila kumpa jaji nafasi ya kuzingatia adhabu mbadala kulingana na mazingira ya kesi husika.

Mahakama imeeleza kuwa utoaji wa adhabu ya kifo kwa lazima unakiuka haki za msingi za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi inayolindwa chini ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ambao Tanzania imeridhia.

Hukumu hiyo ilitolewa jana, Juni 5, 2026, na jopo la majaji wanane wa Mahakama ya Afrika wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Blaise Tchikaya, pamoja na Makamu wa Rais, Chafika Bensaoula.

Maamuzi hayo yametokana na mashauri matatu tofauti yaliyowahusisha wafungwa saba waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji na kusubiri kunyongwa katika magereza mbalimbali nchini.

Waombaji walidai kuwa Tanzania ilikiuka haki zao kadhaa za msingi, zikiwemo haki ya kuishi, utu wa binadamu, kusikilizwa kwa haki, kupata uwakilishi wa kisheria na kusikilizwa kwa mashauri yao ndani ya muda unaofaa.

Kesi ya Chacha Jeremiah

Katika shauri la kwanza, Chacha Jeremiah, Methew Jeremiah Daud na Paschal Ligoye Mashiku, waliokuwa wakitumikia adhabu ya kifo katika Gereza Kuu la Butimba mkoani Mwanza, waliwasilisha maombi ya pamoja namba 039/2019, 040/2019 na 041/2019 mbele ya Mahakama ya Afrika wakitaka itambue kuwa haki zao zilikiukwa.

Katika shauri hilo, walalamikaji walitaka Mahakama iamuru Serikali ya Tanzania iwalipe fidia ya dola za Marekani 10,000 kila mmoja pamoja na nafuu nyingine ikiwemo kuachiliwa huru.

Walidai kuwa adhabu ya kifo ya lazima pamoja na utekelezaji wake kwa njia ya kunyongwa vinakiuka haki zao za kuishi na utu wa binadamu chini ya Ibara ya 4 na 5 za Mkataba wa Afrika.

Pia walieleza kuwa mfumo wa adhabu ya lazima unamnyima jaji mamlaka ya kuzingatia mazingira binafsi ya mshtakiwa na hali halisi ya tukio kabla ya kutoa hukumu.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Mahakama ilikubaliana nao kuwa adhabu ya kifo ya lazima inakiuka haki ya kupata mchakato wa haki kwa sababu inaondoa mamlaka ya mahakama kutumia busara katika utoaji wa adhabu.

Mahakama pia ilibaini kuwa kunyonga kama njia pekee ya utekelezaji wa adhabu ya kifo kunakiuka haki ya utu wa binadamu.

Kutokana na uamuzi huo, Mahakama iliiamuru Tanzania kuondoa adhabu ya kifo ya lazima katika sheria zake, kuondoa kunyonga kama njia ya utekelezaji wa adhabu hiyo, kufuta hukumu za kifo za waombaji hao na kuwaondoa katika orodha ya wafungwa wanaosubiri kunyongwa.

Aidha, ilielekeza mamlaka husika kufanya upya usikilizwaji wa adhabu zao ili majaji waweze kutumia mamlaka yao ya kuamua adhabu kulingana na mazingira ya kila kesi.

Pia Mahakama iliamuru kila mwombaji alipwe fidia ya Sh100,000 kwa madhara ya kimaadili yaliyotokana na ukiukwaji wa haki zao.

Kesi ya Godfrey Gabinus Ndimba

Katika shauri la pili namba 056/2019, Godfrey Gabinus Ndimba pamoja na waombaji wengine wawili waliokuwa wakishikiliwa katika Gereza la Wilaya ya Lindi wakisubiri kunyongwa, walipinga mwenendo wa mashauri yao ya jinai pamoja na adhabu ya kifo waliyopewa.

Miongoni mwa hoja zao kulikuwa na kupinga adhabu ya kifo ya lazima na matumizi ya kunyonga kama njia ya utekelezaji wa adhabu hiyo.

Mahakama iliamua kuwa adhabu ya kifo ya lazima inakiuka Ibara ya 4 ya Mkataba wa Afrika inayolinda haki ya kuishi.

Vilevile, ilibaini kuwa kunyonga kunakiuka Ibara ya 5 inayolinda heshima na utu wa binadamu.

Kutokana na maamuzi hayo, Mahakama iliiamuru Tanzania kufuta hukumu za kifo za waombaji hao, kuwaondoa katika orodha ya wanaosubiri kunyongwa, na kurekebisha sheria zake ili kuondoa adhabu ya kifo ya lazima na kunyonga.

Pia imeitaka kuanza upya hatua za utoaji wa adhabu kwa kuzingatia mamlaka ya jaji kutumia busara.

Kila mwombaji katika shauri hilo alitakiwa kulipwa fidia ya Sh300,000 kwa madhara ya kimaadili.

Kesi ya Masudi Said Selemani

Katika shauri la tatu namba 042/2019, Masudi Said Selemani, aliyekuwa akitumikia adhabu ya kifo katika Gereza Kuu la Lilungu mkoani Mtwara, alipinga hukumu yake pamoja na namna iliyopangwa kutekelezwa.

Selemani alidai kuwa kuhukumiwa adhabu ya kifo bila jaji kupewa nafasi ya kuzingatia mazingira ya kesi yake kulikiuka haki yake ya kuishi.

Pia alieleza kuwa muda mrefu alioutumia akisubiri kunyongwa pamoja na matumizi ya kunyonga kama njia ya utekelezaji wa hukumu vilikiuka haki yake ya utu wa binadamu.

Mahakama ilikubaliana na hoja hizo na kuamua kuwa adhabu ya kifo ya lazima inakiuka Ibara ya 4 ya Mkataba wa Afrika, huku kunyonga na muda mrefu wa kusubiri utekelezaji wa hukumu vikikiuka Ibara ya 5 ya Mkataba huo.

Mahakama iliiamuru Tanzania kuondoa adhabu ya kifo ya lazima na kunyonga katika mfumo wake wa sheria, kufuta hukumu ya kifo dhidi ya Selemani, kumuondoa katika orodha ya wanaosubiri kunyongwa na kufanya upya usikilizwaji wa adhabu yake kwa kuzingatia mamlaka ya jaji kutumia busara.

Selemani pia ametakiwa kulipwa fidia ya Sh300,000 kwa madhara ya kimaadili.

Maagizo kwa Tanzania

Katika hukumu zote tatu, Mahakama ya Afrika ilisisitiza kuwa Tanzania inapaswa kuchukua hatua zote muhimu bila kuchelewa, ikiwemo kurekebisha sheria zake ili kuondoa adhabu ya kifo ya lazima na kunyonga kama njia ya utekelezaji wa adhabu hiyo.

Mahakama pia iliamuru hukumu hizo kuchapishwa katika tovuti za Mahakama ya Tanzania na Wizara ya Katiba na Sheria ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Aidha, Serikali imeagizwa kuwasilisha taarifa kwa Mahakama ya Afrika zikionyesha hatua zilizochukuliwa kutekeleza maamuzi hayo.

Akizungumza baada ya hukumu hizo, wakili wa waombaji, Emanuel Sood, alisema ameridhishwa na uamuzi wa Mahakama kutoa nafuu kuu waliyoomba katika mashauri hayo.

“Jambo kubwa lililopatikana ni amri ya Mahakama kuitaka Tanzania kuondoa adhabu ya kifo ya lazima na kuondoa kunyonga kama njia ya utekelezaji wa adhabu hiyo.”

“Tunaamini hili ni suala ambalo sasa Serikali italazimika kulifanyia kazi,” amesema Sood.

Ameongeza kuwa hukumu hizo zinatarajiwa kuongeza shinikizo kwa Serikali kuoanisha mfumo wake wa haki ya jinai na viwango vinavyoendelea kubadilika vya kikanda na kimataifa katika kulinda haki za binadamu.

WADAU WABAINISHA VIKWAZO VYA UBIA SEKTA YA AFYA KIHONGOSI AKEMEA FITINA NA MAJUNGU KAZINI