SERIKALI YAELEKEZA WALIMU 35 KUPEWA MOTISHA YA VIWANJA
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe ameagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwapatia viwanja walimu 35 waliotunukiwa tuzo za ubora ili kuwapa motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika maeneo yao.
Walimu hao wameibuka vinara kwenye shindano la Taifa la Stadi za Ufundishaji kwa walimu wa elimu ya awali, msingi na sekondari lililoratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa walimu bora Profesa Shemdoe amesema pamoja na zawadi mbalimbali ambapo ziliandaliwa kwa ajili ya washindi wa shindano hilo, Serikali inaona umuhimu wa kuwawezesha kuwa na kumbukumbu ya kudumu ya mafanikio yao kupitia umiliki wa kiwanja katika maeneo wanakofanyia kazi.
Amesema motisha kwa watumishi haitokani na fedha pekee, bali pia mazingira mazuri ya kazi na namna wanavyothaminiwa na waajiri wao.
Akitolea mfano nadharia za utawala na usimamizi wa rasilimali watu, amesema watumishi wanaweza kufanya vizuri zaidi wanapopata mazingira yanayowajengea ari na kuwatambua kwa mchango wao.
“Mtu mmoja aliandika kuhusu nadharia ya utendaji akisema mtumishi hawi motivated kwa pesa pekee yake, bali hata mazingira anayofanyia kazi yanaweza kumhamasisha kufanya vizuri zaidi,” amesema.
Kutokana na msingi huo, Profesa Shemdoe amesema amemuelekeza Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi kufikisha maelekezo rasmi kwa wakurugenzi wa halmashauri zote zinazotoka walimu hao ili kila mmoja apatiwe kiwanja.
“Nawaelekeza wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kwamba wale walimu 35 watakaopata zawadi leo, kama mwalimu ametoka kwenye halmashauri yako, ahakikishiwe anapata kiwanja karibu na makao ya wilaya ili pamoja na zawadi alizopata leo awe na kitu atakachokikumbuka maisha yake yote,” amesema.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza hamasa kwa walimu wengine na kuonesha kuwa Serikali inatambua mchango wao katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Katika hatua nyingine, Profesa Shemdoe ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendeleza mashindano hayo ambayo amesema yamekuwa yakiboreshwa mwaka hadi mwaka na kutoa fursa kwa walimu wengi kuonesha umahiri wao.
“Nimepata taarifa kwamba leo hii ni awamu ya nne. Kulikuwa na awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na sasa tuko awamu ya nne. Hili ni jambo kubwa na zuri sana.Tofauti na miaka ya awali, washiriki wa mwaka huu walituma video zao za ufundishaji ambazo zilifanyiwa tathmini kwa kutumia vigezo maalumu kabla ya kuchaguliwa.
“Hawa wa leo walipeleka video zao na wakafanyiwa tathmini. Mmoja aliambiwa hujafaulu kwa sababu video yako ilikuwa na mapungufu fulani, mwingine akapita kwa sababu alikidhi vigezo. Mpaka kufika hapa walimu 35 kutoka zaidi ya washiriki 3,000 ni kazi kubwa sana,” amesema Profesa Shemdoe.
Amesema mchakato huo umeongeza uwazi na ushindani wa haki, huku ukiwapa walimu nafasi ya kuonesha ubunifu na umahiri wao katika ufundishaji.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Profesa Daniel Mushi amewataka walimu kuendelea kuwa wabunifu, wenye shauku ya kujifunza na tayari kukumbatia mabadiliko yanayoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kuongeza ubora wa elimu na matokeo ya wanafunzi.
Profesa Mushi amesema mafanikio ya mfumo wa elimu hayategemei mitaala au miundombinu pekee, bali yanachangiwa kwa kiwango kikubwa na ubora wa mwalimu aliyepo darasani.
Amesema walimu ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya taifa kwa kuwa wao ndiyo wanaobeba jukumu la kuwaandaa wanafunzi watakaokuja kuwa wataalamu na viongozi wa baadaye.
“Naomba kusisitiza kuwa mafanikio ya mfumo wa elimu hayaamuliwi na mitaala au miundombinu pekee yake, bali yanaamuliwa kwa kiwango kikubwa na ubora wa mwalimu aliyepo darasani. Walimu wetu wote nchini ndio nguzo kuu ya maendeleo ya taifa letu. Walimu mna kila sababu ya kujipigia makofi,” amesema.
Akiwahimiza kuendana na mabadiliko ya dunia, amesema ni muhimu walimu wakaendelea kujifunza mbinu mpya za ufundishaji na kutumia teknolojia katika kuboresha ujifunzaji darasani.
“Naomba niwasihi walimu waendelee kuwa wabunifu, wenye shauku ya kujifunza na wawe tayari kukumbatia mabadiliko yanayoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia,” amesema Profesa Mushi.
Amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika elimu yanaweza kuongeza ufanisi wa ufundishaji na kuwasaidia wanafunzi kupata maarifa yanayolingana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Amesisitiza kuwa kila mwanafunzi anayefaulu, kila ndoto inayotimia na kila mafanikio ya taifa huanzia kwa mwalimu, jambo linaloonyesha nafasi kubwa ya taaluma hiyo katika maendeleo ya nchi.
“Kwa kupitia shindano hili tunaadhimisha ubora, ubunifu na mchango mkubwa wa walimu katika kujenga Tanzania ya leo na Tanzania iliyo bora zaidi ya kesho,” amesema.
Akizungumzia shindano hilo la walimu, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amesema limeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (Mewaka) kwa kutoa fursa kwa walimu kujifunza kwa vitendo, kubadilishana uzoefu na kujiendeleza kitaaluma wakiwa katika mazingira yao ya kazi.
Amebainisha kuwa kupitia mashindano hayo walimu hupata nafasi ya kuonesha umahiri wao wa ufundishaji huku wakijifunza mbinu mpya kutoka kwa wenzao.
“Shindano hili lina nafasi muhimu katika kuimarisha Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini kwa kuwa linatoa fursa kwa walimu kujifunza kwa vitendo, kuonesha umahiri, kubadilishana uzoefu na kuendelea kujiendeleza kitaaluma wakiwa kazini,” amesema.
Ameeleza kuwa walimu wanaoshiriki mashindano hayo hujifunza kutoka kwa wenzao na kuibua mbinu bunifu zinazosaidia kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
“Kupitia shindano hili, walimu hujifunza kutoka kwa wenzao, huibua mbinu bunifu za ufundishaji na kuimarisha matumizi ya mbinu shirikishi, upimaji, Tehama pamoja na matumizi ya zana za kufundishia na kujifunzia,” amesema.
Dk Komba amesema moja ya mafanikio makubwa ya shindano hilo ni kuifanya Mewaka kuwa ya vitendo zaidi kwa kuhakikisha maarifa na uzoefu unaopatikana kwa walimu hauishii kwa washiriki pekee.
Amesema bunifu, maarifa na uzoefu unaozalishwa kupitia shindano hilo hurekodiwa, kuhifadhiwa na kusambazwa kwa walimu wengine kupitia majukwaa mbalimbali ya kujifunzia.