news

WADAU WABAINISHA VIKWAZO VYA UBIA SEKTA YA AFYA

Vardo June 6, 2026 7:05 pm

Dar es Salaam. Kutokuaminiana kati ya Serikali na sekta binafsi, mifumo ya kisheria inayohitaji maboresho, urasimu pamoja na mazingira yasiyotoa uhakika wa uwekezaji ni miongoni mwa vikwazo vya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) kwenye sekta ya afya nchini.

Wadau wa afya wanasema changamoto hizo zimekuwa zikichelewesha utekelezaji wa miradi ya ubia, kupunguza uwekezaji na kuathiri jitihada za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Hayo yameelezwa leo Juni 6, 2026 katika mdahalo wa wadau wa sekta ya afya, uliojadili nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika sekta ya afya kuelekea utekelezaji Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo (FYDP IV) na Dira 2050.

Akizungumza katika mdahalo huo, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema Tanzania haiwezi kufikia malengo yake ya kuwa na mfumo bora wa afya unaotoa huduma kwa wananchi wote, bila kuondoa vikwazo vinavyozuia ushirikiano huo.

Kwa mujibu wa Dk Nkoronko, moja ya changamoto kubwa ni ukosefu wa imani kati ya Serikali na sekta binafsi, hali inayosababisha fursa nyingi za uwekezaji kushindwa kutekelezwa au kuchukua muda mrefu kufikia hatua ya utekelezaji.

“Serikali inawaogopa watu binafsi na sekta binafsi nayo ina wasiwasi na namna itakavyoshirikiana na Serikali. Wakati umefika sasa wa kushughulikia wasiwasi huu na kujenga mazingira ya kuaminiana,” amesema.

Mbali na suala la imani, amesema mifumo ya kisheria na kiutawala wakati mwingine huonekana kuwa migumu na inayozuia kasi ya utekelezaji wa miradi ya ubia.

“Mfumo wa sheria na kanuni unapaswa kuendelea kuboreshwa ili kurahisisha ushirikiano na kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya,” amesema.

Amesema changamoto nyingine ni uhaba wa rasilimali za kifedha zinazohitajika kugharamia uwekezaji katika miundombinu ya afya, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na utoaji wa huduma zinazozidi kuhitajika kutokana na ongezeko la watu na mabadiliko ya magonjwa.

Kilio wazalishaji wa dawa

Kwa upande wao, wazalishaji wa dawa nchini wameeleza kuwa pamoja na umuhimu wa ubia, bado mazingira ya uwekezaji yanahitaji maboresho ili kuvutia mtaji zaidi katika sekta ya afya.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Viwanda vya Dawa Tanzania (TPMA), Bashiru Haroon amesema mafanikio ya sekta hiyo yatategemea zaidi ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wawekezaji kuliko ushindani kati ya pande hizo mbili.

Amesema moja ya changamoto inayowakabili wawekezaji ni pale ambapo Serikali inaingia katika maeneo ambayo tayari sekta binafsi imewekeza na kuyafanya kama shughuli za kibiashara.

“Tunachokiomba ni kuhakikisha Serikali inakuwa mwezeshaji wa uwekezaji badala ya kuwa mshindani wa wawekezaji. Tunahitaji mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kufanya kazi kwa ufanisi na kuendelea kuwekeza,” amesema.

Miongoni mwa mapendekezo yake ni Serikali kuweka mikataba ya muda mrefu ya ununuzi wa dawa zinazozalishwa nchini kupitia hospitali zake na mfumo wa bima ya afya kwa wote ili kuwapa wawekezaji uhakika wa soko.

Ubia kuongeza tija

Mkurugenzi wa Kituo cha PPP, David Kafulila amesema PPP ni moja ya njia muhimu zitakazosaidia Tanzania kuboresha huduma za afya, kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya tiba, kuvutia teknolojia mpya na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema sekta binafsi tayari imekuwa mshirika mkubwa wa Serikali katika utoaji wa huduma za afya, huku hospitali, zahanati na vituo vya afya vinavyomilikiwa na watu binafsi vikichangia kwa kiasi kikubwa kupanua huduma kwa wananchi.

“Fikiria hali ingekuwaje kama sekta binafsi isingekuwapo katika huduma za afya. Serikali inatambua mchango mkubwa wa wawekezaji binafsi katika kujenga na kuendesha hospitali, kununua vifaa tiba na kutoa huduma zinazowafikia wananchi kila siku,” amesema.

Alitumia nafasi hiyo kuzitaka halmashauri, wizara na taasisi za umma kuweka bayana fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo yao, ili kuwapa wawekezaji binafsi taarifa sahihi zitakazowawezesha kuibua na kuandaa miradi ya ubia.

ZANZIBAR YAGEUKIA TEKNOLOJIA YA SRI NA UHIFADHI SHIRIKISHI KUNUSURU MISITU, KUONGEZA TIJA KATIKA MISITU MAHAKAMA YA KITAIFA YAIAMURU TANZANIA KUONDOA ADHABU YA KUNYONGWA