MSIMU UJAO HATARINI KWA YAKOUB BAADA YA UPASUAJI WA GOTI
KIPA wa Simba, Yakoub Suleiman, anakabiliwa na kipindi kigumu cha kuuguza jeraha baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti, hali inayotarajiwa kumuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu na huenda akakosa sehemu kubwa ya msimu ujao.
Yakoub amekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo tangu alipoumia akiwa na timu ya taifa ya Niger wakati wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) yaliyofanyika nchini Morocco.
Tangu wakati huo, ameshindwa kurejea katika kiwango chake bora na kuendelea kusumbuliwa na maumivu ya mara kwa mara.
Awali, kipa huyo alifuata matibabu ya kawaida kwa matumaini ya kupona bila kufanyiwa upasuaji.
Hata hivyo, baada ya kufanyiwa uchunguzi na tathmini ya kina ya kitabibu, ilibainika kuwa njia hiyo haikutoa matokeo yaliyokusudiwa, hivyo kulazimika kukubali kufanyiwa upasuaji ili kupata suluhisho la kudumu.
Yakoub alijiunga na Simba akitokea JKT Tanzania kama mbadala wa Moussa Camara, lakini maisha yake ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi yamekuwa na changamoto nyingi kutokana na majeraha yaliyomzuia kuonyesha uwezo wake kwa kiwango cha juu.
Tangu kutua Simba, amefanikiwa kucheza mechi chache za Ligi Kuu Tanzania Bara, huku mchezo wake wa mwisho ukiwa dhidi ya Azam FC mnamo Desemba 12, 2025, ambapo Simba ilipoteza kwa mabao 2-0.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa upasuaji wake umefanyika kwa mafanikio na kwa sasa anaendelea na programu maalumu ya matibabu pamoja na mazoezi ya kurejesha utimamu wa mwili chini ya usimamizi wa jopo la madaktari.
Akizungumzia hali ya kipa huyo, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, amesema Yakoub hataweza kucheza tena msimu huu na kuna uwezekano mkubwa wa kuukosa pia sehemu ya msimu ujao kutokana na muda unaohitajika kwa ajili ya kupona kikamilifu na kurejea katika kiwango cha ushindani.
Kukosekana kwa Yakoub ni pigo kwa Simba, hasa ikizingatiwa kuwa kabla ya kuandamwa na majeraha alikuwa ameonyesha kiwango kizuri, akiruhusu mabao matano pekee katika mechi tisa za mwanzo alizocheza akiwa langoni mwa Wekundu wa Msimbazi.