RUSHINE SIO BEKI TU, NI MWALIMU WA MASINDE SIMBA
BEKI wa kati wa Simba, Vedastus Masinde, amemtaja beki mwenye uzoefu mkubwa, Rushine De Reuck, kuwa miongoni mwa watu waliomsaidia kwa kiasi kikubwa kuonyesha kiwango bora tangu ajiunge na kikosi hicho cha Msimbazi.
Masinde amesema amejifunza mambo mengi tangu aanze kucheza sambamba na Rushine, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwake ndani na nje ya uwanja.
Beki huyo, ambaye anacheza msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kujiunga na Simba akitokea TMA FC, amesema uwepo wa Rushine umekuwa kama darasa muhimu kwake kutokana na uzoefu mkubwa alioupata alipokuwa akiichezea klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa Masinde, Rushine ni mfano bora wa nidhamu, kujituma na kujitolea katika kazi, sifa ambazo zimekuwa zikimsaidia kupiga hatua katika maendeleo yake ya soka la ushindani.
“Beki huyo mwenye uzoefu mkubwa huwa hashindwi kutoa ushauri. Mara nyingi hutumia hata mazoezini kuonyesha namna ya kukabiliana na washambuliaji wa kiwango cha juu kana kwamba tunacheza mechi rasmi,” amesema Masinde.
Ameongeza kuwa hali hiyo humhamasisha kuongeza juhudi kila siku na kumfanya kutambua kuwa mafanikio ya mchezaji yanatokana na kujituma kwa kiwango cha juu katika kila kipindi cha mazoezi.
Mbali na uwezo wake ndani ya uwanja, Masinde amebainisha kuwa Rushine pia ni mfano wa kuigwa katika maisha ya kawaida, akizingatia ratiba za mazoezi, lishe bora na mapumziko ya kutosha.
Anaamini kuendelea kujifunza kutoka kwa wachezaji wenye uzoefu kama Rushine kutamsaidia kufikia malengo yake makubwa ya soka, huku akiwahimiza vijana wengine kufuata misingi ya nidhamu, kujituma na kujifunza kutoka kwa waliowatangulia ili kutimiza ndoto zao.