MKENYA AINGIA ANGA ZA AZAM FC
UONGOZI wa Azam FC unaendelea na mchakato wa kuboresha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, ambapo kwa sasa inafuatilia saini ya beki wa kulia wa Kenya Police FC ya Kenya, Mkenya Daniel Sakari Macheso.
Azam imeanza mchakato wa kutafuta beki wa kulia wa kwenda kuongeza ushindani kwa nahodha wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda baada ya mshindani wake, Nathaniel Chilambo anayemaliza mkataba wake msimu huu kudaiwa anakaribia kujiunga na Simba.
Taarifa kutoka Kenya zinaeleza beki huyo amekuwa kivutio kikubwa kwa timu mbalimbali za nje ya nchi hiyo, huku Azam ikiwa ni miongoni mwa klabu zinazomuhitaji, japo hakuna makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili.
Ofisa Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Azam FC, Rashid Seif alisema ni mapema kuzungumzia suala la usajili kwa sababu bado msimu haujaisha, kwa sasa malengo ni kumaliza vizuri mechi zilizobakia.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua Azam imeanza mchakato wa kutafuta beki wa kulia wa kusaidiana na nahodha Lusajo, baada ya kutokuwa na uhakika wa kuendelea na Chilambo anayedaiwa tayari amesaini Simba.