DUCHU ASEMA UKWELI MCHUNGU KWA WAPINZANI, SIMBA INAJITAZAMA YENYEWE
BEKI wa Simba SC, David Kameta ( Duchu), amesema kikosi hicho hakina muda wa kufuatilia wapinzani wao wanafanya nini katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, badala yake nguvu zote zimeelekezwa katika kuhakikisha wanashinda mechi zao zilizosalia.
Duchu amesema Simba bado ipo kwenye nafasi nzuri ya kupigania taji la ligi msimu huu licha ya ushindani mkubwa uliopo, huku akisisitiza kuwa kila mchezaji anatambua wajibu wake katika kipindi hiki muhimu cha mwisho wa msimu.
“Nina imani kubwa Simba inaweza kuchukua ubingwa. Msimu uliopita tofauti ilikuwa pointi tatu, lakini safari hii bado kuna tofauti ya alama mbili huku zikiwa zimebaki mechi tano,” amesema Duchu.
Beki huyo ameongeza kuwa jambo muhimu kwa sasa si kuangalia matokeo ya wapinzani wao, bali kuhakikisha Simba inafanya kazi yake kwa usahihi ndani ya uwanja.
“Msimu huu ni mgumu sana, lakini maono ya Simba kutwaa ubingwa yapo wazi kwa sababu tunahitaji kushinda mechi zote tano zilizobaki. Hatuna muda wa kuangalia wengine wanafanya nini au kusikiliza mambo yao,” amesema
Duchu amesisitiza kuwa hatima ya mbio za ubingwa itajulikana mwishoni mwa msimu, hivyo Simba inapaswa kubaki makini na kupambana katika kila mchezo.
“Kikubwa ni kufanya kazi yetu, kuwa makini katika michezo yetu na kuhakikisha tunapata ushindi. Mambo mengine yataamuliwa mwisho wa msimu,” amesema Duchu.
Kauli hiyo inaonyesha dhamira ya wachezaji wa Simba ya kupambana hadi dakika ya mwisho katika mbio za ubingwa, huku wakiamini ushindi katika mechi zao zilizobaki unaweza kuwafikisha kwenye lengo lao la kutwaa taji la Ligi kuu