YANGA YABANWA NA SIMBA, MWAMNYETO ASEMA KAZI BADO HAIJAISHA
NAHODJA wa Yanga SC, Bakari Nondo, amesema mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bada zimezidi kuwa ngumu, hivyo kila timu inapaswa kuhakikisha inashinda mechi zake zilizobaki ili kufikia malengo yake.
Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 60 baada ya kucheza mechi 25, ikifuatiwa kwa karibu na Simba SC yenye pointi 58. Tofauti ya pointi mbili pekee kati ya timu hizo imeongeza ushindani mkubwa katika vita ya kuwania taji la msimu wa 2025/26.
Timu zote zimecheza mechi 25 na zimesaliwa na michezo mitano kabla ya kufungwa kwa pazia la msimu huu, huku Yanga ikiwa na jukumu la kutetea ubingwa wake.
Akizungumzia hali ya ushindani ilivyo kwa sasa, Nondo alisema kila mchezo uliobaki una umuhimu mkubwa kwa timu zinazowania nafasi za juu.
“Tunatambua ushindani ni mkali na kila timu inapambana kufikia malengo yake. Kikubwa kwa sasa ni kuhakikisha kila mmoja anashinda mechi zake,” amesema Nondo.
Ameongeza kuwa Yanga inakabiliwa na michezo migumu katika hatua za mwisho za msimu, lakini wachezaji wamejipanga kupambana kwa nguvu zote ili kupata matokeo chanya.
“Tuna mechi ngumu mbele yetu, lakini tutapambana kupata matokeo mazuri. Hilo ni jukumu letu kama wachezaji, na tunaomba mashabiki waendelee kuwa nasi katika nyakati zote,” ameongeza.
Yanga itashuka dimbani katika mchezo wake ujao dhidi ya Mashujaa FC utakaochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, ambapo mabingwa hao watetezi watahitaji ushindi ili kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la ligi.