SIMBA YA LEO NA SIMBA YA KESHO ZINAJENGWA KWA MSINGI IMARA
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo imejikita katika kujenga mfumo endelevu wa kuzalisha vipaji na viongozi wa benchi la ufundi watakaoweza kuendeleza falsafa ya timu kwa miaka mingi ijayo.
Ahmed amesema mpango huo unafanana na dhana ya succession inayotumiwa na klabu kubwa duniani, ambapo huandaliwa mrithi wa kuendeleza mafanikio na utamaduni wa timu bila kuyumba pale mabadiliko yanapotokea.
Akizungumzia maendeleo ya timu za vijana,
Ahmed ameeleza kuwa Simba imewekeza muda, fedha na imani kubwa kwa kocha John Bocco, akisisitiza kuwa lengo ni kuandaa watu wa ndani watakaokuwa walinzi wa utamaduni na falsafa ya klabu.
“Simba ya leo na Simba ya kesho lazima iwe na mwendelezo. Tumekuwa tukiwekeza kwa makusudi ili kuandaa watu wetu wenye uwezo wa kurithi na kuendeleza yale ambayo klabu inayaamini,” amesema Ahmed.
Amefananisha mkakati huo na ule wa baadhi ya klabu kubwa za dunia ambazo zimefanikiwa kupitia mfumo wa kuandaa warithi.
Ametolea mfano namna kocha Mikel Arteta alivyonufaika na uzoefu alioupata kabla ya kupewa majukumu makubwa, huku akitaja pia mifano ya makocha waliopita katika mifumo ya klabu kubwa za Ulaya na kuendelea kufanya vizuri.
Ahmed ameongeza kuwa kwa sasa Simba inanufaika na mchango wa Selesmani Matola ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa makocha mbalimbali wanaokuja ndani ya klabu kutokana na uelewa wake wa mazingira, utamaduni na falsafa ya timu.
Kwa mujibu wa Ahmed, mkakati huo ni sehemu ya safari ya Simba kuelekea kujenga taasisi imara inayotegemea mfumo badala ya watu binafsi, jambo ambalo linaifanya klabu kuwa na uhakika wa mafanikio ya sasa na ya baadaye.