BARKER AICHARUKIA LIGI, AWEKA SIMBA MSTARI WA UBINGWA MECHI 5 ZILIZOBAKI
KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema maandalizi ya kikosi chake kuelekea mechi tano za mwisho za Ligi Kuu Tanzania Bara yanaendelea vizuri, huku akisisitiza umuhimu wa timu hiyo kujikita zaidi katika malengo yake ya msimu.
Barker amesema timu hiyo ilirejea mazoezini wiki iliyopita na tangu wakati huo mazoezi yamekuwa yakifanyika kwa mpangilio mzuri na wenye tija, hali inayoonesha mwendelezo chanya kuelekea hatua ya mwisho ya ligi.
Amefafanua kuwa kiwango cha utimamu wa wachezaji kinaendelea kupanda siku hadi siku, huku benchi la ufundi likiendelea kufanya tathmini ya kina kuhakikisha Simba inakamilisha msimu ikiwa katika hali bora zaidi kiufundi na kimwili.
“Kwa sasa bado tunawakosa baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa, lakini ninatarajia kurejea kwao kutaongeza nguvu kwenye maandalizi yetu kabla ya kuingia kwenye ratiba ngumu ya mwisho wa msimu,” amesema Barker.
Amesema kurejea kwa nyota hao kutaleta ushindani mkubwa ndani ya kikosi, jambo analoliona kuwa muhimu sana katika kipindi hiki ambacho kila mchezo una uzito mkubwa kwenye mbio za ubingwa.
Akizungumzia ushindani wa kileleni mwa msimamo wa ligi, Barker amesema hana muda wa kuangalia wapinzani wake wanafanya nini, bali anachotaka ni kuona Simba inatekeleza majukumu yake ipasavyo na kupata matokeo chanya katika mechi zilizosalia.
Ameongsza kuwa lengo kuu la benchi la ufundi ni kuhakikisha Simba inamaliza msimu kwa nguvu na kufikia malengo iliyojiwekea bila kuyumba katika safari ya mwisho ya mashindano.