Yanga SC

KAMWE AFICHUA SIRI YA YANGA KABLA YA KUIKABILI MASHUJAA FC

Vardo June 9, 2026 8:50 pm

OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kikosi cha timu hiyo kinatarajia kuondoka Alhamisi kuelekea Kigoma kwa ajili ya maandalizi ya mchezo muhimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC utakaochezwa Juni 13, 2026.

Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na dhamira ya kusaka alama tatu muhimu zitakazoiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kuongoza mbio za kutetea taji la ligi msimu huu.

Akizungumza kuhusu hali ya kikosi, Kamwe amesema maandalizi yanaendelea vizuri chini ya benchi la ufundi, huku wachezaji wote wakionyesha utayari mkubwa wa kuikabili Mashujaa FC.

Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kurejea kwa baadhi ya nyota waliokuwa nje kutokana na majeraha, akiwemo beki na nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein maarufu kama Zimbwe Jr.

Kamwe amesema Zimbwe Jr ameshapona na kwa sasa yuko katika hali nzuri ya ushindani, jambo linalompa kocha Abdihalim Moalin chaguo zaidi kuelekea mchezo huo muhimu.

“Timu inaendelea na mazoezi na baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi wamerejea, akiwemo Zimbwe Jr ambaye alikuwa hajaonekana kwa muda mrefu kutokana na majeraha. Kwa sasa yupo fiti na atakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza dhidi ya Mashujaa FC,” amesema Kamwe.

 

Pamoja na kujiamini, Kamwe amesisitiza kuwa mchezo dhidi ya Mashujaa FC hautakuwa mwepesi, akieleza kuwa Yanga inahitaji kupambana kwa nguvu zote ili kupata ushindi na kuendelea kujijengea mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

BARKER AICHARUKIA LIGI, AWEKA SIMBA MSTARI WA UBINGWA MECHI 5 ZILIZOBAKI SLOTOPIA IPO MERIDIANBET KUGEUZA MUDA WAKO KUWA USHINDI