YANGA YAPIGA HODI KWA BEKI HATARI IVORY COAST
KATIKA kuhakikisha wanaimarisha safu ya ulinzi kuelekea msimu ujao, uongozi wa Yanga umeanza hatua za awali za kutafuta mbadala wa beki wao wa kushoto, Chadrack Boka, ambaye anatarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa macho ya Yanga yameelekezwa kwa beki wa kushoto wa Mouna FC ya Ivory Coast, Samba Koné, anayekadiriwa kuwa miongoni mwa mabeki wenye kiwango bora katika ligi ya nchi hiyo kwa sasa.
Koné, mwenye umri wa miaka 23, ameonekana kuwa chaguo sahihi kwa mabosi wa Yanga kutokana na uwezo wake wa kucheza kwa ufanisi katika majukumu ya ulinzi na kusaidia mashambulizi, jambo ambalo limewavutia viongozi wa klabu hiyo.
Faida nyingine kwa Yanga ni kwamba mkataba wa beki huyo na Mouna FC unatarajiwa kumalizika Juni 30 mwaka huu, hali inayoweza kurahisisha mazungumzo ya usajili na kupunguza gharama za kumpata.
Mbali na kucheza nchini Ivory Coast, Koné pia ana uzoefu wa soka la Afrika Kaskazini baada ya kuwahi kuitumikia Paradou FC ya Algeria kwa mkopo kabla ya kurejea katika klabu yake ya sasa.
Msimu huu, beki huyo ameonyesha kiwango cha kuvutia akiwa amechangia asisti nne, huku akitajwa miongoni mwa mabeki bora wa kushoto katika Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Taarifa hizo zimeongeza imani kwa Yanga kuwa anaweza kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na kutoa mchango mkubwa.
Iwapo mazungumzo kati ya pande hizo yatafikia makubaliano, Samba Koné huenda akawa mmoja wa usajili wa kwanza wa Yanga katika dirisha lijalo, huku klabu hiyo ikijipanga kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya mashindano ya ndani na ya kimataifa msimu ujao.