NJIA YA SIMBA KUFANIKIWA SIO KUANGALIA YANGA
KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema hana utamaduni wa kuilinganisha timu yake na klabu nyingine, ikiwemo watani wao wa jadi Yanga SC.
Akisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuhakikisha Simba inaendelea kupiga hatua na kufikia malengo iliyojiwekea.
Barker alitoa kauli hiyo kuhusu tofauti kati ya Simba na Yanga, timu ambazo zimekuwa zikishindana kwa karibu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi katika miaka ya karibuni.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema mafanikio ya Simba hayatategemea kile kinachofanywa na wapinzani wao, bali namna ambavyo timu yake itatekeleza mipango na mikakati yake kwa usahihi ndani na nje ya uwanja.
Ameeleza kuwa jambo muhimu kwa sasa ni kuendelea kuijenga Simba kuwa timu bora zaidi kila siku, huku akiwataka wachezaji wake kubaki na umakini mkubwa ili kuhakikisha malengo ya msimu huu yanafikiwa.
“Mimi binafsi sipendi sana kutulinganisha na timu yoyote kwenye ligi. Jambo muhimu ni kuzingatia kile tunachotaka kufanikisha sisi wenyewe,” amesema Barker akieleza falsafa yake ya uongozi ndani ya klabu hiyo.
Barker ameongeza kuwa Simba ina malengo makubwa ya kupigania ubingwa wa ligi na wakati huohuo kuendelea kujenga heshima yake katika mashindano ya kimataifa, hasa katika soka la Afrika ambako ushindani unaongezeka kila mwaka.
Kauli hiyo inakuja wakati Simba ikiendelea na maandalizi ya michezo yake ijayo ya Ligi Kuu, huku mashabiki wa klabu hiyo wakisubiri kuona timu yao ikiendeleza kiwango kizuri na kuimarisha harakati za kusaka mataji msimu huu.