Singida Big Stars FC

STRAIKA MKONGOMANI AITEKA SINGIDA BLACK STARS

Vardo June 9, 2026 8:09 am

MABOSI wa Singida Black Stars wanaendelea kufanyia tathimini maeneo ya kuboresha msimu ujao, ambapo kwa sasa inaangalia uwezekano wa kuinasa saini ya mshambuliaji nyota Mkongomani Gusto Wa Ilungo Mulongo anayeichezea Vipers SC ya Uganda.

Mshambuliaji huyo aliyezaliwa Februari 21, 2004, huko DR Congo, ni miongoni mwa vijana wenye vipaji vikubwa ambapo kwa sasa ameanza kuvutia timu mbalimbali nje ya Uganda, huku kwa upande wa Tanzania Singida ikiwa mstari wa mbele kumtaka.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa Singida, kimeliambia Mwanaspoti kuwa Gusto ni pendekezo la Kocha, Mkongomani Papy Kimoto anayemuhitaji kikosini humo, japo hata ikiwa usajili wake utakamilika atatolewa kwa mkopo ili akapate uzoefu kwingine.

“Gusto ni mchezaji kijana mwenye kipaji kikubwa lakini endapo tutakamilisha usajili wake tunaweza kumtoa kwa mkopo kwa timu nyingine ili akapate nafasi zaidi ya kucheza, mazungumzo yameanza ila bado hayajakamilika,” kilisema chanzo hicho.

Kocha Mkuu wa Singida, Muhibu Kanu alipoulizwa amesema kikosi hicho kitafanya maboresho kama ilivyo kawaida kila msimu unapoisha kwa lengo la kuongezea nguvu timu, japo hadi sasa ni mapema kwa sababu wanapambana kuhakikisha wanamaliza vizuri mechi zote.

“Benchi la ufundi litakuwa na ripoti yake tutakayoiwasilisha msimu ujao kwa lengo la kufanyiwa maboresho, ila kwa sasa ni mapema kueleza mipango iliyopo, tunachotaka ni kumaliza msimu vizuri ili tufuzu Michuano ya Kimataifa,” amesema Kanu.

Kanu alianza kushika nafasi hiyo ya kocha mkuu wa Singida tangu Aprili 5, 2026, baada ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho Mkenya David Ouma kuondoka kutokana na mwenendo usioridhisha, hasa katika Ligi Kuu Bara kwa mechi za msimu wa 2025-2026.

Hata hivyo, uongozi wa Singida ulimtangaza Kimoto kuwa meneja mkuu wa timu hiyo na Kapiten Ngoyi Dora akiwa ni kocha msaidizi wake, huku makocha wote wawili wakisaini mkataba wa mwaka mmoja na miezi mitatu kikosini.

Kimoto amejiunga na Singida akiwa na uzoefu wa kutosha wa kufundisha soka kwa ngazi ya klabu alioupata kwa kuzinoa timu tano tofauti za DR Congo, ambazo ni AS Maniema Union, OC Renaissance, FC Saint-Eloi Lupopo, JS Kinshasa na AS Dragons.

Kocha huyo ana leseni Daraja A ya CAF inayomuwezesha kukaa benchi katika mashindano ya Klabu Afrika na hata timu za Taifa.

NJIA YA SIMBA KUFANIKIWA SIO KUANGALIA YANGA NSAJIGWA KATIKA MTIHANI MPYA TANZANIA PRISONS