NSAJIGWA KATIKA MTIHANI MPYA TANZANIA PRISONS
IKIWA ni mara ya kwanza kuongoza timu ya Ligi Kuu akiwa Kocha Mkuu, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ anaingia katika mtihani wa kusaka rekodi na heshima mpya katika medani za soka nchini akiwa na Tanzania Prisons.
Nsajigwa aliyewahi kuzitumikia Tanzania Prisons, Yanga na Taifa Stars kwa sasa ndiye Kocha Mkuu wa Maafande hao baada ya kuaminiwa na Jeshi la Magereza kuiongoza kwa mechi zilizobaki.
Kocha huyo mwenye Diploma A ya CAF, alikabidhiwa kibarua hicho akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Zedekiah Otieno raia wa Kenya ambaye alionekana kuzidiwa baada ya kuongoza takribani mechi 12.
Beki huyo wa zamani na mzaliwa wa mkoani Mbeya, anakuwa kocha wa tatu katika misimu mitatu mfululizo kutwishwa jukumu la kuwa kocha mkuu wa Tanzania Prisons, akifuata nyayo za Ahmad Ally wa JKT Tanzania na Aman Josiah wa Dodoma Jiji.
Kwa sasa Tanzania Prisons imebakiza michezo mitano kujua hatma yake na katika mechi 25 ilizocheza imekusanya pointi 20 na kuwa nafasi ya 15 na kuweka presha kwenye hesabu za kukwepa kushuka daraja.
Mwanaspoti imemchambua kocha huyo mzawa na mtihani alionao wa kumvusha au kumkwamisha katika kazi yake iwapo atafuata nyayo za makocha wenzake waliotambulishwa Ligi Kuu na sasa wanang’ara.
Historia ya Prisons misimu mitatu
Pamoja na msoto wa matokeo mazuri kwa misimu mitatu, Prisons imekuwa sehemu ya daraja kwa kuwatambulisha makocha wazawa na kuwapa njia ya mafanikio.
Msimu wa 2023/24 timu hiyo ilianza na Kocha Fredi Felix ‘Minziro’ ambaye aliiongoza kwa takribani michezo tisa na kuvuna pointi saba na kuwa nafasi ya 14.
Baada ya hapo, mabosi wa timu waliamua kumtema na kumpa nafasi Ahmad Ally aliyetokea KMC.
Ally akiwa KMC alikuwa Kocha Msaidizi na kwa mara ya kwanza alitambulishwa na Tanzania Prisons kumpa heshima ya Kocha Mkuu. Aliweza kufanya vizuri akikumbukwa kuwazamisha Simba mabao 2-1 Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Baada ya matokeo mazuri na kuiacha salama Prisons, alisajiliwa na JKT Tanzania ambako ameendelea kufanya vizuri.
Ahmad kabla ya kutua JKT Tanzania alikuwa amepita Marsh Queens, Mbao FC akiwa msaidizi pamoja na KMC akiwa chini ya makocha Ettiene Ndayiragije na Hitimana Thiery.
Prisons haikuishia hapo ilipoamua kumpa kazi Aman Josiah ambaye hakuwa na jina kubwa kwenye medani za soka licha ya uzoefu alionao.
Josiah aliyewahi kuzinoa Biashara United ya Mara na Tunduru Korosho, kwa sasa ndiye Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji.
Kocha huyo alitambulishwa rasmi msimu wa 2024/25 baada ya kuitwa kuziba nafasi ya Mbwana Makata aliyesitishiwa mkataba kutokana na matokeo mabaya.
Makata aliiongoza timu hiyo katika michezo 14 akivuna pointi 11 katika nafasi ya 15 na vigogo wa timu wakaona busara kumtema na kumpa kazi Josiah aliyekuwa Geita Gold ya Championship.
Kwa sasa Josiah ni miongoni mwa makocha bora kwenye Ligi Kuu kufuatia uwezo alioonesha kwa Dodoma Jiji kwani mbali na timu nyingi kukumbana na kipigo kwake, Yanga ni sehemu ya watakaomkumbuka.
Yanga msimu huu ilikuwa haijapoteza mchezo wowote kabla ya kuzimwa mabao 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji, huku Simba wao wakiambulia suluhu katika mchezo wa awali.
Mtihani wa Nsajigwa
Kwa sasa akili na macho ya wadau na mashabiki wa soka jijini Mbeya wanamtazama nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars kuona kama ataweza kuinusuru timu hiyo ambayo hali yake si shwari kwenye Ligi Kuu.
Nsajigwa bado hajawa na matokeo mazuri kwani katika michezo 10 aliyoongoza timu hiyo ameshinda miwili, sare mbili na kupoteza sita hali inayompa wakati mgumu kuinusuru timu kutoshuka daraja.
Matarajio ya wengi ni kuwa iwapo kocha huyo ataibakiza Prisons Ligi Kuu huenda ikawa njia yake ya kujitangaza na pengine kumpaisha kama walivyofanya Josiah na Ahmad Ally.
Hata hivyo, Prisons imekuwa na misimu migumu hivi karibuni ikiponea kushuka daraja ikiwamo kucheza play-off ilipoitoa JKT Tanzania kwa jumla ya mabao 2-1 na kubaki salama.
Mwenyewe anasemaje?
Kwa nyakati tofauti kocha huyo amekuwa akitoa matumaini ya kubakiza timu hiyo licha ya kukiri ugumu wa ligi na mipango yake na benchi la ufundi ni kuhakikisha wanakwepa aibu hiyo.
Anabainisha kuwa licha ya ligi kusimama, ameamua kuvunja mapumziko ya wachezaji kuendelea na mazoezi ili kuboresha na kusahihisha makosa kwa lengo la kushinda mechi zilizobaki.
“Ligi imekuwa ngumu lakini kazi ya kocha ni kufundisha na ndilo ninalofanya na ninaamini kwa ari na morali ya wachezaji ilivyo na namna walivyoamua kujitolea timu itabaki salama.
“Hizi mechi tano zilizobaki ni kufa na kupona, lazima tutokwe jasho ukizingatia hatutaki sare wala kupoteza, ushindi wa mchezo dhidi ya Pamba ulitupa matumaini na nguvu mpya kikosini,” anasema Nsajigwa.
Mastaa wakaza
Straika wa timu hiyo, George Mpole anasema kwa sasa kilichobaki ni juhudi binafsi na kupambania timu kwa kila mchezo kuhakikisha wanabaki salama na kulinda heshima yao kikosini.
“Hakuna kilichobaki zaidi ya kupambania timu, kila mmoja anayo ari na morali ya kufa na kupona kuhakikisha tunabaki salama. Wachezaji maazimio ni kuona kuanzia mechi ijayo na Dodoma Jiji tunashinda,” anasema kinara huyo wa mabao sita kikosini.
Straika mkongwe Samson Mbangula anasema wachezaji wakiwamo wazoefu wanashirikiana vyema na wale wageni na chipukizi kuhakikisha wanashinda mechi zilizobaki.
“Kwa sasa lengo ni moja tu, timu ibaki. Sisi wazoefu kwenye timu tunao ushirikiano na mazungumzo ya kunusuru timu isishuke daraja, tunaamini kwa umoja wetu tutafikia lengo,” anasema Mbangula.
Uongozi nao
Ofisa Habari wa timu hiyo, Alexander Ngelela amesema hadi sasa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Jeremiah Katungu ametangaza bonasi nono kwa wachezaji ikiwa ni hamasa kwa timu kufanya vizuri katika mechi tano zilizobaki.
Bila kutaja kiwango, Ngelela amesema mbali na bonasi hiyo, kigogo huyo ametoa vibali kwa watumishi wa jeshi hilo kutoka zaidi ya mikoa tisa ili kusafiri kuishangilia timu hiyo popote itakapocheza kuanzia mechi dhidi ya Dodoma Jiji.
“Tunamshukuru Kamishna Jenerali ametoa bonasi katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji na tukipoteza hatutakuwa na excuse, hata wachezaji wanaitaka mechi, hivyo uongozi tumejipanga,” anasema Ngelela.