GEITA GOLD, KAGERA SUGAR ZILISTAHILI KUREJEA LIGI KUU
GEITA Gold na Kagera Sugar zimerejea Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao wa 2026-2027, baada ya kujihakikishia ushindi katika mechi zao za raundi ya 28 na zimezifanya kufikisha pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine zozote.
Ushindi wa Geita Gold wa mabao 3-1, dhidi ya Songea United kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, umeifanya kufikisha pointi 71, ikiwa ndio vinara baada ya kushinda mechi 22, sare tano na kupoteza moja, huku Kagera Sugar ikifikisha pointi 68.
Kagera ilifikisha pointi hizo 68 na kujihakikishia rasmi kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya maafande wa Polisi Tanzania kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Mbuni FC na kuishia pointi 60, ambazo hata ikishinda mechi zote mbili itaishia na pointi 66.
Timu hizo zilianza kuonyesha matumaini ya kurejea tena Ligi Kuu Bara tangu mwanzo wa ligi kutokana na ushindani waliouonyesha, kama ambavyo Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa kina na kile ilichokifanya hadi kupanda.
GEITA GOLD
Baada ya Geita Gold kudumu Championship kwa siku 740, ambazo ni sawa na miaka miwili na siku 10 au miezi 24 na siku 10, hatimaye kikosi hicho kimerejea tena Ligi Kuu Bara, baada ya kushinda mabao 3-1, dhidi ya Songea United.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Nyankumbu, Geita, mabao hayo ya timu hiyo yalifungwa na nyota wa kikosi hicho, Maulid Shaban aliyefunga mawili, huku lingine moja likifungwa na Richardson Ng’ondya na kupeleka shangwe kikosini humo.
Geita inayofundishwa na Kocha, Zubery Katwila ilishuka daraja msimu wa 2023-2024 na ushindi huo wa juzi umeifanya kufikisha pointi zake 71, ambazo zimeihakikishia kumaliza nafasi mbili za juu katika msimamo wa ligi, na ni kinara ikiwa na pointi 71, baada ya kushinda mechi 22, sare tano na kupoteza moja tu kati ya 28.
Geita ilishuka Championship baada ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu Bara nafasi ya 15 na pointi 25, baada ya kushinda mechi tano, sare 10 na kupoteza 15, ikiungana na Mtibwa Sugar iliyomaliza ya 16 na pointi 21, japo imesharejea.
Mechi ya mwisho kwa timu hiyo iliyohitimisha safari yake ya Ligi Kuu Bara, ilipigwa Mei 28, 2024 na ilichapwa mabao 2-0 na Azam FC kwa mabao ya Yeison Fuentes na Feisal Salum ‘Fei Toto’, ikitimiza siku 740, za majonzi na furaha.
Msimu uliopita wa 2024-2025 wa Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, ikiwa na aliyekuwa Kocha Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.
Timu hiyo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu dhidi ya Stand United, ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudiwa ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.
REKODI YA KIPEKEE
Rekodi bora ya Geita Gold msimu huu ni kutopoteza mechi yoyote nyumbani msimu huu wa 2025-2026, kwani timu hiyo imecheza 14, imeshinda 11 na kutoka sare tatu, ikifunga mabao 40 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.
Kwa upande wa mechi za ugenini, timu hiyo imecheza pia 14, imeshinda 11, sare mbili na kupoteza moja tu, ikifunga mabao 23 na kuruhusu 7, ikikusanya pointi 35, ambazo ni moja zaidi ya nyumbani ambayo ilikusanya pointi 36.
Geita ndio timu iliyopoteza mechi chache za msimu huu na kikosi hicho kimechapwa mara moja tu, kati ya 28, ikiwa ni kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Polisi Tanzania, mechi iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi, Februari 20, 2026.
MSIMU WA KUKUMBUKWA
Katika msimu bora na wa kukumbukwa kwa Geita na wadau wa soka, ni ule wa 2021-2022, ambao timu hiyo ilishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, jambo lililoiwezesha kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Geita ilimaliza ya nne na pointi 46, baada ya kushinda mechi 12, sare 10 na kupoteza minane, nyuma ya Azam FC iliyokuwa ya tatu na pointi 49, Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 61 na mabingwa kwa msimu huo, Yanga, iliyokusanya pointi 74.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, Geita iliposhiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023, ilitolewa raundi ya kwanza kwa faida ya bao la ugenini, baada ya sare ya kufungana mabao 2-2, dhidi ya Hilal Alsahil ya Sudan.
Mechi ya kwanza iliyopigwa Sudan, Geita Gold ilichapwa bao 1-0, japo, ziliporudiana jijini, Dar es Salaam, Kwenye Uwanja wa Azam Complex, kikosi hicho kilishinda mabao 2-1, hivyo, kuwafanya Wasudan kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.
REKODI YA MSIMU WA MWISHO
Timu hiyo haikuwa na rekodi nzuri katika msimu wake wa mwisho wa Ligi Kuu ambao ni wa 2023-2024, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kushuka daraja, ingawa, kwa msimu huu kwenye Championship, Katwila ameitengeneza kuleta ushindani.
Msimu wa 2023-2024, Geita ilimaliza nafasi ya 15 na pointi 25 Ligi Kuu, baada ya kushinda mechi tano, sare 10 na kupoteza 15 na safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ilifunga mabao 18, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 38.
Kwa msimu huo, Geita ilishuka daraja na Mtibwa Sugar iliyoburuza mkiani na pointi 21, baada ya kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza 19, ingawa, imerejea tena Ligi Kuu, kufuatia kutwaa ubingwa wa Championship msimu wa 2024-2025.
GEITA YA PILI KWA KATWILA
Katwila ameandika rekodi nyingine mpya ya kuipandisha Geita Gold Ligi Kuu Bara, ikiwa ni timu ya pili kwake pia kufanya hivyo, baada ya msimu wa 2019-2020 kupanda na Ihefu SC ya jijini Mbeya na kwa sasa inajulikana kama Singida Black Stars.
Hata hivyo, Katwila anakuwa ni kocha wa pili kuipandisha Geita Gold Ligi Kuu, baada ya Fredy Felix ‘Minziro’ aliyepo kwa sasa Fountain Gate aliyekipandisha pia kikosi hicho msimu wa 2021-2022, akiendelea kukumbukwa na wadau wa soka wa Geita.
KAGERA SUGAR
Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20, tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.
Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, amekirejesha tena kikosi hicho baada ya mwenendo mzuri tangu mwanzo wa msimu.
HAIJAPOTEZA NYUMBANI
Rekodi nyingine bora kwa Kagera Sugar msimu huu ni ya kutopoteza mechi yoyote nyumbani kama ilivyokuwa kwa Geita Gold, kwani kikosi hicho kimecheza 13 na kimeshinda 10 na kutoka sare tatu, huku kikifunga mabao 27 na kuruhusu matano.
Katika mechi hizo 13 za nyumbani, timu hiyo imekusanya pointi 33, huku kwa zile za ugenini ikicheza 15 na kati ya hizo imeshinda 11, sare mbili na kupoteza mbili, ikifunga mabao 25 na kuruhusu saba, ikiwa imekusanya pointi zake 35.
WASIKIE MAKOCHA
Akizungumza na Soka la Bongo, Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zubery Katwila anasema siri kubwa ya mafanikio hayo ni ushirikiano kutoka kwa viongozi na wachezaji tangu mwanzo wa msimu, licha ya changamoto ya ushindani mkubwa wa Championship.
“Mbali na ushirikiano wetu ila moja ya jambo kubwa nililolitaka kwa viongozi ni kuhakikisha tunakuwa na wachezaji bora watakaotupigania kuanzia mwanzo hadi mwisho, nashukuru viongozi walizingatia na tumefanikiwa pamoja,” anasema Katwila.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja aliyewahi kutamba na timu za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, anasema wachezaji walitambua umuhimu wa kuipambania klabu hiyo irejee, baada ya makosa yaliyojitokeza msimu uliopita.