Habari za michezo

MAKOCHA WAKABILIWA NA MAAMUZI MAGUMU YA VIKOSI KOMBE LA DUNIA

Vardo June 11, 2026 9:10 am

MEXICO CITY, MEXICO: HOMA ya Kombe la Dunia sasa imeikumba dunia huku timu kutoka nchi 48 zikiwa njiani au ndani ya Marekani, Mexico na Canada kwa ajili ya mashindano makubwa zaidi kuwahi kuandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Makocha wanaweka mipango yao sawa ya mwisho kabla ya raundi ya kwanza ya mechi za makundi, lakini kwa baadhi bado kuna uamuzi mkubwa wa kufanya.

Kwa kueleweka kabisa baadhi ya timu zinazotajwa kuwa miongoni mwa zinazopigiwa upatu kutwaa ubingwa zina wingi wa vipaji katika nafasi fulani, hivyo kuamua ni wachezaji gani waanze na ni nani anafaa kuingia kutokea benchi limekuwa jambo gumu. Wakati huohuo, mashabiki pia wanataka kuona mambo makubwa huku wakitumaini timu zao zitafika hadi fainali itakayochezwa New Jersey, Julai 19.

Kwa hiyo, ni maumivu gani makubwa ya vichwa vya uteuzi wa vikosi inapofika mechi ya ufunguzi leo, Juni 11? Na ni mijadala gani ambayo mashabiki na vyombo vya habari wanaijadili katika baadhi ya mataifa yenye matarajio makubwa zaidi? GOAL imechambua sita kati ya mijadala inayovutia zaidi.

England: Jude vs Rogers

Kocha Thomas Tuchel ana uamuzi kadhaa wa kufanya kabla ya kutaja kikosi chake cha England kitakachocheza dhidi ya Croatia katika mechi ya ufunguzi ya Kundi L, lakini kinachovutia zaidi ni pambano kati ya Jude Bellingham na Morgan Rogers kuanza kama kiungo mshambuliaji zaidi katika safu ya viungo ya Three Lions nyuma ya Harry Kane.

Bellingham pamoja na Kane ndiyo taswira inayotambulika zaidi England, lakini baada ya msimu usioridhisha akiwa Real Madrid na huku kukiwa na maswali kuhusu uhusiano wake na Tuchel, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 yupo katika hatari ya kuanza mashindano akiwa benchi.

Badala yake, Tuchel anaweza kuamua kumtumia Rogers pamoja na Declan Rice na Elliot Anderson. Nyota huyo wa Aston Villa anatoka kwenye msimu bora ambapo alifunga mabao 14 yakiwa ni mengi ya mashuti ya mbali ya kuvutia na kutoa asisti 11 kwa mabingwa wa Europa League.

Rogers aliivutia England katika mechi za kufuzu wakati Bellingham alipokuwa akipona upasuaji wa bega, huku katika mechi mbili tangu mwanzo wa msimu ambapo wote wawili walikuwa tayari kucheza, kila mmoja akianza mara moja. Kati ya wawili hao, Bellingham ndiye aliyetoa kiwango kilichovutia zaidi katika ushindi dhidi ya New Zealand majuzi wakati Tuchel alipohakikisha kila mchezaji wa kikosi chake anapata dakika 45 za kuongeza utimamu wa mwili. Mechi ya jana, Jumatano dhidi ya Costa Rica huenda ikawa imetoa dalili zaidi kuhusu mawazo ya Mjerumani huyo.

Hispania: Nani aanze golini?

Kwa upande wa uamuzi ambao kocha Luis de la Fuente atafanya, utambulisho wa kipa wa kwanza wa Hispania katika Kombe la Dunia unaonekana upo tayari. Hata miongoni mwa mashabiki wa La Roja, hakuna mjadala mkubwa sana kuhusu suala hilo. Lakini mashabiki wa Ligi Kuu England hasa watakapogundua kuwa David Raya siyo kipa namba moja wa taifa lake, wengi watakuwa wanauliza kwa nini.

Unai Simon amekuwa kipa chaguo la kwanza wa Hispania tangu Euro 2020, na kipa huyo wa Athletic Bilbao anatarajiwa tena kuvaa glovu Amerika Kaskazini licha ya kiwango bora alichoonyesha Raya akiwa Arsenal, ambako alishinda Golden Glove EPL kwa misimu mitatu mfululizo.

Raya alitunza rekodi ya kutofungwa katika mechi 28 kati ya 51 alizoichezea Arsenal msimu uliopita, na alionekana na wengi kuwa kipa bora zaidi Ulaya katika kipindi hicho. Kwa Hispania, hata hivyo, ameanza mechi moja tu ikiwa ni ya kirafiki dhidi ya Misri tangu Novemba 2024, na hakika atakuwa kipa wa akiba wa Simon Hispania itakapoanza kampeni yake dhidi ya Cape Verde.

“Itakuwa siyo haki kama hatutathamini ubora, hadhi, historia na uzoefu wa kitaaluma wa Unai Simon,” alisema De la Fuente alipoulizwa kuhusu makipa wake mwezi Machi. “Itakuwa jambo la kipuuzi kwangu kuja hapa na kulazimika kuthibitisha hilo tena, kwa sababu tu yeye ni Unai Simon. Kipa anapokuwa katika kiwango hiki, lazima uheshimu hadhi yake na historia yake.”

Na kwa mashabiki wa Barcelona wana matumaini kwamba Joan Garcia angepewa nafasi baada ya msimu wake bora wa kwanza Camp Nou. Hata hivyo, kiwango chake kisichoridhisha katika sare ya wiki iliyopita dhidi ya Irak kimeua matumaini yoyote ya kumbadilisha mawazo De la Fuente.

Brazil: Vita straika wa kati

Huenda hakuna nafasi duniani inayokuja na presha kubwa zaidi kuliko kuwa mshambuliaji wa kwanza wa Brazil katika Kombe la Dunia, na licha ya mechi ya ufunguzi ya Selecao dhidi ya Morocco kuwa chini ya wiki moja, bado kuna mjadala kuhusu nani ambaye kocha Carlo Ancelotti atamchagua New Jersey hasa baada ya kumuacha nje ya kikosi chake cha mwisho mshambuliaji aliyekuwa akitarajiwa kuanza, Joao Pedro wa Chelsea. Matheus Cunha amepewa jezi namba 9 kwa mashindano hayo na, baada ya kuanza katika ushindi wa kirafiki dhidi ya Panama, anaonekana kuwa mbele ya wengine. Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Manchester United ana bao moja tu la kimataifa katika mechi 13, huku uwezo wake wa kucheza pembeni au kama namba 10 ukifanya baadhi ya watu waone siyo mshambuliaji wa asili.

Mchezaji anayefaa zaidi maelezo hayo ni Igor Thiago, ambaye aliibuka ghafla na kujipatia nafasi katika kikosi cha Ancelotti baada ya msimu wa kushangaza akiwa Brentford. Ni Erling Haaland pekee aliyefunga mabao mengi zaidi Ligi Kuu England kuliko Thiago alivyofunga msimu uliopita, na tayari amefunga mabao mawili katika mechi nne za kwanza za Brazil. Kuna maswali kuhusu mchezo wake wa jumla, lakini hakuna shaka kwamba anajua njia ya kwenda golini. Mwingine wa tatu ni mchezaji ambaye wengi walitarajia tayari angekuwa amejihakikishia nafasi ya mshambuliaji namba 9 tangu alipoibuka miaka miwili iliyopita, Endrick. Hata hivyo, baada ya kupata nafasi chache Real Madrid, ‘Pele mpya’ alipoteza nafasi yake katika timu ya taifa, na bila mkopo wake wa kujiimarisha akiwa Lyon katika nusu ya pili ya msimu wa 2025-26 pamoja na majeraha ya washambuliaji wengine, huenda asingerejea kwenye mawazo ya Ancelotti.

Yupo kikosini hata hivyo, na ameonyesha kiwango kizuri tangu kurejea kwake. Katika dakika 13 tu dhidi ya Croatia mwezi Aprili, Endrick alipata penalti na kutoa asisti iliyosaidia ushindi, kabla ya kufunga bao lake la kwanza la kimataifa kwa karibu miaka miwili katika ushindi dhidi ya Misri, Jumamosi. Lakini je, kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 amefanya vya kutosha kujipatia nafasi ya kuanza? Tutajua Jumamosi.

Argentina: Alvarez au Lautaro au wote?

Mabingwa watetezi Argentina wanaingia katika Kombe la Dunia wakiwa na karibu kikosi kilekile kilichotwaa ubingwa Qatar 2022, huku wachezaji kadhaa wakongwe wakiongozwa na Lionel Messi wakitarajiwa kucheza mashindano yao ya mwisho duniani. Hata hivyo, eneo moja litakaloonekana tofauti kidogo ni safu ya ushambuliaji baada ya kustaafu kwa Angel Di Maria. Akiwa na Di Maria kushoto na Messi kulia, Julian Alvarez aliibuka kuwa mshambuliaji wa kwanza wa La Albiceleste. Hata hivyo, kiwango cha Lautaro Martinez katika miaka miwili iliyopita kinaweza sasa kumtoa mchezaji huyo wa Atletico Madrid katika nafasi hiyo, ingawa haimaanishi atatoka kabisa kwenye kikosi cha kwanza.

Lautaro alimaliza mfungaji bora wa Copa America 2024 licha ya kuanza mechi mbili tu, na amefunga mabao 15 katika mechi 20 za mwisho za kimataifa, huku akiendelea kuwa na rekodi bora ya mabao akiwa Inter Milan. Kwa upande mwingine, Alvarez amefunga mabao saba katika mechi 20 za mwisho za Argentina, na ingawa alifanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa Atletico Madrid msimu uliopita, alifunga mabao mawili tu La Liga tangu mwanzo wa Oktoba. Kocha Lionel Scaloni anataka kuwaingiza wote wawili kikosini, na suluhisho linaonekana kuwa kumchezesha Alvarez upande wa kushoto, Lautaro katikati na Messi upande wa kulia.

Ufaransa: Nafasi ya Cherki ni ipi?

Rayan Cherki hana upungufu wa kujiamini. Akizungumza baada ya Ufaransa kushangazwa kwa kufungwa na Ivory Coast katika mechi ya kwanza ya kirafiki kabla ya mashindano, kiungo mshambuliaji huyo wa Manchester City alisema: “Hatuendi Kombe la Dunia kama vipenzi vya ubingwa, bali kwenda kuwashinda vibaya kila mtu.” Cherki huenda alikuwa katika hali nzuri baada ya kufunga bao na kushangiliwa kwa kusimama alipofanyiwa mabadiliko huko Nantes, lakini kauli zake zilisababisha mjadala mkubwa katika vyombo vya habari vya Ufaransa na zimemlazimisha kocha Didier Deschamps kufafanua kuwa kikosi chake hakiendi Amerika Kaskazini kikiwa na kiburi. Hii siyo mara ya kwanza Cherki kumpa Deschamps maumivu ya kichwa, kwani kocha huyo yupo chini ya presha ya kumtafutia nafasi mmoja wa vipaji vya kipekee zaidi katika safu yake ya ushambuliaji iliyojaa nyota.

Ujerumani: Chaguo kwa namba 9

Ukosefu wa mshambuliaji wa kuaminika umeikwamisha Ujerumani kwa zaidi ya nusu muongo, na kocha Julian Nagelsmann yupo chini ya presha kufanya uchaguzi sahihi wa mshambuliaji huku Die Mannschaft wakitaka kuepuka kutolewa katika hatua ya makundi kwa mara ya tatu mfululizo.

Nagelsmann angalau ana chaguo zuri, huku Kai Havertz akiwa mbele kwa sasa. Mchezaji huyo wa Arsenal alifunga bao na kutoa asisti dhidi ya Marekani Jumamosi, na pia alifunga dhidi ya Ghana mwezi Machi. Nick Woltemade alianza katika mechi hiyo, na mwanzoni mwa mwaka alikuwa kipenzi cha wengi kuanza majira haya ya kiangazi baada ya kufunga mabao manne katika mechi sita za kufuzu za Ujerumani. Hata hivyo, nusu ya pili ya msimu isiyoridhisha akiwa Newcastle United huenda ikamfanya abaki benchi.

Lakini, mpinzani mkuu wa Havertz si Woltemade. Heshima hiyo inamwendea Deniz Undav, ambaye mashabiki wengi wa Ujerumani wanaamini anapaswa kuanza baada ya msimu ambao ulimshuhudia akifunga mabao 25 na kutoa asisti 14 katika mashindano yote akiwa Stuttgart. Undav ana rekodi bora ya ufungaji kwa taifa lake, na mabao yake mawili dhidi ya Finland mwishoni mwa Mei yalifikisha kuwa sita katika mechi tisa. Bila shaka ndiye mchezaji mwenye kiwango bora zaidi kati ya watatu hao linapokuja suala la kufunga mabao. Iwapo ataweza kumuondoa Havertz na uzoefu wake wa mechi kubwa, bado inabaki kuonyesha uwanjani.

 

MOALLIN ACHEKELEA MABAO YA DUBE,DEPU TAHADHARI KALI KWA MASHABIKI WANAOSAFIRI KOMBE LA DUNIA