MOALLIN ACHEKELEA MABAO YA DUBE,DEPU
KUNA ukame uliowapitia washambuliaji wawili wa Yanga, Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ sasa jamaa wametupia huko timu za taifa na kumfanya kocha wao Abdihamid Moalin amechekelea akisema ni hatua nzuri.
Dube alifungia Zimbabwe kwenye mechi mbili za kalenda ya FIFA dhidi ya India, mchezo uliopigwa Mei 30. Dube mwenye mabao tisa hajaifungia Yanga kwenye mechi tano zilizopita.
Wakati Depu alifunga bao lake dhidi ya Afrika ya Kati na kuisaidia Angola kushinda kwa mabao 3-0.
Depu mwenyewe hajaiofungia Yanga kwenye mechi saba zilizopita tangu alipofunga dhidi ya Prisons.
Akizungumzia hatua hiyo kocha Moalin alisema amefurahishwa na hatua ya washambuliaji hao kumaliza ukame akisema sasa hatua hiyo itawarudishia morali na kuajiamini wakati wakirudi kuendelea kuitumikia Yanga.
Moalin alisema bado benchi lake lina imani na washambuliaji hao wawili na kwamba hatua wanayopitia ni kawaida kwenye soka lakini ubora wao upo palepale.
“Ni hatua nzuri tumeona ndio wameanza kufunga, ukiwa kocha au mtu unayeipenda klabu hii hakika utafurahia kitu cha namna hii, nadhani sasa ni wakati mzuri watarudi klabuni wakiwa na morali tena umeifungia timu yako ya taifa,”alisema Moalin.
“Watarudi wakiwa wanajiamini sasa, tutaendelea kuwapa nafasi kama ambavyo ilikuwa kabla kwa kuwa ni washambuliaji wetu na tunawaamini, unajua kwenye soka nyakati kama hizi ni kawaida kuna wakati unarudi chini na hili halidumu linapita na unarudi kufanya vizuri.
“Tuna mechi ngumu tano zimesalia kumaliza msimu tunafurahia kila mchezaji amerudi salama na wamefanya vizuri.”