Yanga SC

KILA MECHI NI FAINALI, MOALLIN ASEMA YANGA TAYARI KUIKABILI MASHUJAA

Vardo June 12, 2026 3:08 pm

KOCHA Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC utakaopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma, na amesisitiza kuwa kila mechi iliyobaki ni fainali katika harakati za kutwaa ubingwa wa tano mfululizo.

Moallin amesema maandalizi ya timu yamekwenda vizuri wakati wa mapumziko ya dirisha la FIFA, jambo lililowapa nafasi ya kujiandaa vyema kwa michezo iliyosalia msimu huu.

Amesema wachezaji wake wana hamasa kubwa na wako tayari kurejea kwa nguvu kwenye kampeni za ligi.
“Kwanza kabisa, maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea mchezo wa kesho.

Tulikuwa na kipindi kizuri cha mapumziko ambapo tulipata muda mzuri wa maandalizi. Ninafurahi kuona wachezaji wangu wana hamasa kubwa na wako tayari kurejea kwenye mechi za mwisho za ligi,” amesema Moallin.

Kocha huyo amebainisha kuwa licha ya kuipa heshima Mashujaa FC kama ilivyo kwa timu nyingine zote, Yanga imewasili Kigoma ikiwa na lengo moja tu la kuhakikisha inapata ushindi na kuendelea kujiimarisha katika mbio za ubingwa.

Amesisitiza kuwa hakuna mchezo mwepesi katika Ligi Kuu Tanzania Bara, akieleza kuwa kila timu inapambana kwa malengo yake na hivyo Yanga inalazimika kuingia uwanjani kwa umakini mkubwa katika kila mechi.

“Hakuna mchezo rahisi katika ligi hii. Haijalishi tunacheza na timu ya mwisho kwenye msimamo au timu ya pili, kila mchezo kwetu ni fainali. Lengo letu ni kutwaa ubingwa wa tano mfululizo na kila mchezo ni hatua muhimu kuelekea kufanikisha azma hiyo,” amesema.

Moallin pia amewapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kuonyesha nidhamu, kujituma na kubaki na ari ya ushindani licha ya presha kubwa ya mbio za ubingwa.

Amewashukuru mashabiki wa Yanga wa Kigoma kwa mapokezi makubwa waliyoipa timu tangu ilipowasili mkoani humo.

KOCHA MKWASA AUNGWE MKONO SERIKALI YAPANIA MAKUBWA 2026/27 KWENYE MICHEZO