Michezo

SERIKALI YAPANIA MAKUBWA 2026/27 KWENYE MICHEZO

Vardo June 12, 2026 3:22 pm

SERIKALI imeweka mkakati wa kuibadilisha taswira ya michezo nchini ikilenga kuipandisha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kutoka nafasi ya 112 katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwaka 2025 kuingia katika orodha ya timu 50 bora duniani kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Lengo hilo limeainishwa katika vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 uliowasilishwa jana Alhamisi, Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Hatua hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kutumia michezo kama nyenzo ya kukuza vipaji, ajira, uchumi na hadhi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa. Mbali na kulenga mafanikio katika viwango vya Fifa, Serikali pia imeweka shabaha ya Tanzania kupanda kutoka nafasi ya 25 hadi nafasi ya tano katika viwango vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ifikapo mwaka 2026/27.

Endapo malengo hayo yatafikiwa, Tanzania itakuwa miongoni mwa mataifa yenye ushawishi mkubwa zaidi wa soka Afrika.

Katika soka la wanawake, Serikali imeonyesha azma ya kufanya mapinduzi kwa kulenga kupandisha timu za taifa za wanawake kutoka nafasi ya 145 hadi 40 katika bora za FIFA.

Aidha, katika viwango vya CAF, Tanzania inalenga kutoka nafasi ya 30 hadi nafasi ya 10 bora barani Afrika.

Mpango huo pia unaweka mkazo katika kukuza michezo ya kitaalamu kwa kuongeza idadi ya wachezaji wa kiume wanaoshiriki michezo ya kulipwa kutoka 1,200 hadi 1,560, ifikapo 2026/27.

Kwa upande wa wanawake, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kutoka 250 hadi 400, jambo linalotarajiwa kuongeza fursa za ajira, maendeleo ya vipaji na ushindani wa kimataifa.

Sambamba na michezo, Serikali imeainisha malengo ya kuimarisha sekta za sanaa na ubunifu. Idadi ya wasanii wa muziki wa Tanzania wanaopokea tuzo inatarajiwa kuongezeka kutoka 17 mwaka 2024/25 hadi 20 mwaka 2026/27, huku wadau wa filamu wanaopokea tuzo za kimataifa wakitarajiwa kuongezeka kutoka 86 hadi 95 katika kipindi hicho.

Aidha, miradi ya filamu inayopata mikopo inatarajiwa kuongezeka kutoka 137 hadi 183, wakati sekta za ubunifu na maudhui ya kidijitali zikilenga kufikia wadau 1,500 kutoka 1,211.

Serikali pia inalenga kuongeza kiwango cha wasanii na mashirika ya michezo yanayonufaika na mirabaha kutoka asilimia 20 mwaka 2024 hadi asilimia 35 ifikapo 2026/27.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Dk. Seif Muba alisema ni jambo zuri kuweka matarajio lakini yanapaswa kuendana na uhalisia.

“Tunapoweka makadirio ni lazima yaendane na uhalisia. Kama tumefikiria kwa usahihi nadhani tumefanya makadirio makubwa sana. Tuweke makisio ambayo tunayamudu.

“Kwangu naona sio rahisi kuvuka kutoka nafasi ya 112 hadi ya 50. Turudi kwenye nia iwe kuongeza ufanisi katika timu zetu za taifa, zipunguze hilo pengo ambalo lipo dhidi ya timu nyingine. Tunaweza kuanza na hawa Serengeti Boys tukasema miaka nane ijayo wacheze Kombe la Dunia. Tukafanya uwekezaji hapo.”

KILA MECHI NI FAINALI, MOALLIN ASEMA YANGA TAYARI KUIKABILI MASHUJAA CHUKWU MLANGO WA KUTOKEA SINGIDA BS