Simba SC

SIMBA YAKAMILIKA, PAMBA JIJI KATIKA HATARI KUBWA

Vardo June 12, 2026 10:06 am

KIKOSI cha Simba SC kinachonolewa na Kocha Mkuu, Steve Barker, kimeanza maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji FC, huku kikijipanga kurejea kwenye mawindo kwa nguvu kubwa na dhamira ya kuvuna alama tatu muhimu.

Simba inatarajiwa kushuka dimbani Jumapili, Juni 14, 2026, katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, kuwakaribisha Pamba Jiji FC katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Baada ya mapumziko yaliyotokana na majukumu ya timu za taifa, mabingwa hao wa kihistoria wanarejea vitani wakiwa na lengo la kuendelea kujiimarisha katika mbio za kuwania mafanikio ya ligi msimu huu.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema hali ya kikosi ni nzuri na benchi la ufundi limeanza maandalizi maalum kuhakikisha timu inapata ushindi katika mchezo huo.

Ahmed amesema wachezaji wote waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa tayari wamerejea kambini na wanaendelea na mazoezi bila matatizo yoyote ya kiafya.

“Wachezaji wote waliokuwa katika majukumu ya timu za taifa wamerejea na wako fiti. Tunaingia kwenye mchezo wetu wa Jumapili dhidi ya Pamba Jiji tukiwa tumekamilika kwa asilimia 100 na tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Ahmed.

Kwa mujibu wa Simba, maandalizi yanaendelea vizuri huku wachezaji na benchi la ufundi wakionyesha ari kubwa ya kuhakikisha wanaendeleza kasi yao ya ushindani na kuwapa furaha mashabiki wao kwa kupata alama tatu muhimu mbele ya Pamba Jiji FC.

BACCA NA MWAMNYETO WAPEWA DHAMANA YA KULINDA POINTI TATU YANGA KATIKA HATARI YA KUFUNGIWA USAJILI, FIFA SAA 45 ZA MAAMUZI