BACCA NA MWAMNYETO WAPEWA DHAMANA YA KULINDA POINTI TATU
KAZI kubwa ipo kwa safu ya ulinzi ya Yanga kuhakikisha inakuwa imara na makini katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Mabeki wa Yanga wanatarajiwa kuwa na jukumu la kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao na kuhakikisha Mashujaa FC hawapati nafasi za kufika katika eneo hatari na kutengeneza nafasi za mabao.
Safu hiyo ya ulinzi inayoongozwa na Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Israel Patrick Mwenda na Yao Kouassi itahitaji kuwa katika kiwango bora ili kuisaidia timu kuondoka na matokeo chanya katika mchezo huo wa ugenini.
Kocha Mkuu wa Yanga, Abdilhamid Moalin, ameendelea kusuka kikosi chake kuelekea pambano hilo, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu ya kiuchezaji na umakini katika kila idara ya timu, hususan safu ya ulinzi.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri na kikosi kipo katika hali nzuri ya ushindani kuelekea mechi hiyo muhimu.
Kamwe amesema benchi la ufundi lina imani na uwezo wa wachezaji wake, akieleza kuwa kila idara ya timu kuanzia ulinzi, kiungo hadi ushambuliaji ipo tayari kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Umoja wa wachezaji na benchi letu la ufundi unatupa imani kubwa ya kupata alama tatu katika mchezo wetu dhidi ya Mashujaa FC,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa hakuna mchezaji mwenye tatizo la majeraha, huku wote waliopo Kigoma wakiwa fiti na tayari kuipambania Yanga katika harakati za kusaka ushindi utakaoiwezesha kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi na kuimarisha azma ya kutetea ubingwa wao.