Yanga SC

YANGA KATIKA HATARI YA KUFUNGIWA USAJILI, FIFA SAA 45 ZA MAAMUZI

Vardo June 12, 2026 10:17 am

KLABU ya Yanga imejikuta katika wakati mgumu baada ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kutoa uamuzi unaowataka kulipa TP Mazembe ya DR Congo kiasi cha dola za Marekani 43,000 pamoja na riba katika kesi inayomhusu aliyekuwa mshambuliaji wao, Jean Baleke.

Uamuzi huo unatokana na mgogoro wa kimkataba ulioibuka kufuatia usajili wa Baleke, ambaye aliitumikia Yanga kwa mkopo akitokea TP Mazembe.

Klabu hiyo ya DR Congo ilifungua shauri FIFA ikidai kuwa Yanga walishindwa kutekeleza baadhi ya majukumu ya kifedha yaliyokuwa sehemu ya makubaliano ya usajili huo.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Yanga italazimika kulipa dola 43,000 kama deni kuu, huku kiasi hicho kikiongezewa riba kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na FIFA.

Mbali na deni hilo, FIFA pia imeiwekea Yanga faini ya dola 10,000 pamoja na gharama za kisheria za dola 5,000, jambo linaloongeza mzigo wa kifedha kwa mabingwa hao wa Tanzania.

Aidha, FIFA imeagiza kuwepo kwa riba ya asilimia tano kwa mwaka kwenye deni hilo hadi litakapolipwa kikamilifu. Hali hiyo ina maana kuwa kuchelewa kwa malipo kutasababisha ongezeko la gharama kwa klabu hiyo.

Katika uamuzi wake, FIFA imeipa Yanga siku 45 kutekeleza malipo yote yaliyoainishwa.

Endapo klabu hiyo itashindwa kutimiza agizo hilo ndani ya muda uliopangwa, itakabiliwa na adhabu ya kuzuiwa kufanya usajili kwa madirisha matatu mfululizo ya usajili.

Iwapo adhabu hiyo itaanza kutekelezwa, inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mipango ya Yanga ya kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao, hasa wakati ambao klabu hiyo inajiandaa kushiriki mashindano ya ndani na yale ya kimataifa

SIMBA YAKAMILIKA, PAMBA JIJI KATIKA HATARI KUBWA BEN POL, KAMERA ZINAFICHA MENGI NYUMA YETU