Burudani

MWISHO WA SAFARI YA MZEE ONYANGO, AACHA WATOTO 10, WAJUKUU 12, NA VITUKUU 12

Vardo June 13, 2026 8:26 pm

Huzuni, simanzi na kumbukumbu za mchango mkubwa katika sanaa ndivyo vilivyotawala eneo la Kawe jijini Dar es Salaam wakati mamia ya waombolezaji walipokusanyika kumuaga mwigizaji mkongwe wa filamu nchini, Issa Joseph Mohamed ‘Mzee Onyango’, aliyefariki dunia, Juni 11, 2026.

Miongoni mwa viongozi waliojitokeza kutoa heshima za mwisho kwa mkongwe huyo wa sanaa alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, ambaye aliwasili pamoja na mkewe Mariam Mwinyi.

Uwepo wa Rais Mwinyi ulionyesha namna Onyango alivyokuwa na heshima kubwa katika jamii.

Baada ya shughuli ya kuaga mwili wake, Rais Mwinyi aliungana na ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wasanii katika safari ya kwenda Makaburi ya Kondo yaliyopo Ununio, Dar es Salaam, ambako marehemu alizikwa.

Mzee Onyango ameacha watoto 10, wajukuu 12 na vitukuu 12.

Akizungumza wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa marehemu, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema Tanzania imepoteza mmoja wa wasanii walioweka msingi imara katika tasnia ya maigizo.

Amesema licha ya kusimama mbele ya waombolezaji kuzungumza, moyoni alikuwa amejawa na huzuni kubwa kutokana na mchango wa Mzee Onyango katika maendeleo ya sanaa nchini.

“Mzee Onyango alikuwa mpendwa wa watu wengi. Leo tunaona umati mkubwa wa waombolezaji uliokusanyika hapa kwa sababu aligusa maisha ya watu wengi kupitia kazi zake za sanaa,” amesema.

Ameongeza kuwa Mzee Onyango alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa sanaa ya maigizo katika redio na kuyapeleka kwenye televisheni, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa tasnia ya filamu nchini.

“Mara nyingi watu walidhani ni raia wa nchi jirani kutokana na lafudhi na namna alivyocheza baadhi ya nafasi zake. Lakini ukweli ni kwamba alikuwa Mtanzania halisi na mcheshi hadi siku zake za mwisho,” amesema.

Mwakilishi wa familia, Devotha Helman, aliwashukuru Watanzania waliokuwa pamoja na Mzee Onyango katika kipindi chake cha ugonjwa na wale waliojitokeza kwenye msiba.

Amesema familia imeguswa na upendo mkubwa ulioonyeshwa na wananchi, viongozi, wasanii pamoja na madaktari wa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo waliomhudumia katika siku zake za mwisho.

“Kutoweka kwake kumeacha pengo kubwa sana katika familia na jamii kwa ujumla. Tunamuomba Mungu amlaze mahali pema peponi mzee wetu Onyango,” amesema.

WASANII WAMKUMBUKA

Muigizaji Jay B amesema amejifunza mengi kutoka kwa Mzee Onyango na kwamba, alikuwa mmoja wa watu waliomsaidia kufanya mabadiliko kutoka maigizo redioni kwenda kwenye televisheni.

“Nitamkumbuka kwa mambo mengi. Tumefanya kazi pamoja katika filamu mbalimbali na alikuwa mtu aliyependa kuona wasanii vijana wanapiga hatua,” amesema.

Ameongeza kuwa kifo kimekatisha baadhi ya mipango yao ya kazi ikiwamo filamu mpya ambayo walikuwa wameanza kuijadili kabla ya mauti kumfika.

Kwa upande wake, mwigizaji Steve Nyerere amesema msanii huyo ameacha funzo kubwa kwa wasanii kutokana na bidii na mapenzi yake katika sanaa hadi mwisho wa maisha yake.

“Alikuwa mtu wa kazi. Hata alipokuwa amezeeka bado alikuwa tayari kushiriki shughuli za sanaa. Hilo ni somo kubwa kwa kizazi cha sasa,” amesema.

UMATI WAMUAGA

Kuanzia nyumbani kwa marehemu Kawe hadi makaburini Ununio, waombolezaji walionekana wengi wakishiriki shughuli za mazishi.

Wasanii wa maigizo walikuwa miongoni mwa makundi yaliyojitokeza kwa idadi kubwa zaidi, jambo lililoonyesha heshima aliyokuwa nayo marehemu katika tasnia hiyo.

Ibada ya kuaga mwili wake ilichukua muda mrefu kutokana na idadi kubwa ya watu waliotaka kutoa heshima za mwisho.

Mzee Onyango alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni 12, 2026 katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa mtoto wake, Joseph Issa, msanii huyo alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu (presha) kwa muda mrefu, huku hali yake ikibadilika mara kwa mara.

Kifo chake kimehitimisha safari ya mmoja wa waigizaji waliotoa mchango mkubwa katika historia ya maigizo nchini, huku wengi wakimkumbuka kama msanii aliyebeba tabasamu la Watanzania kwa miongo kadhaa na kusaidia kufungua njia kwa kizazi kipya cha waigizaji nchini.

DAKIKA 1,080 MTIBWA SUGAR BILA USHINDI UGENINI MSIMU WA MABINGWA WAFUNGULIWA MERIDIANBET KASINO