Yanga SC

BAADA YA KUIFUNGA MASHUJAA, YANGA YAHAMISHIA VITA ARUSHA

Vardo June 14, 2026 3:42 pm

OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema ushindi walioupata dhidi ya Mashujaa ni hatua muhimu katika mbio za ubingwa, lakini bado hawajajitangaza mabingwa kwa kuwa ligi haijamalizika na kuna mechi nne zilizobaki ambazo zina jumla ya pointi 12 za kuwania.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kamwe amesema kikosi hicho kimefanikiwa kutimiza lengo la kupata alama tatu muhimu sambamba na kutoruhusu bao, jambo ambalo linaonyesha uimara wa timu katika kipindi hiki muhimu cha msimu.

Ameleza kuwa kila mchezo uliosalia una uzito mkubwa kutokana na ushindani uliopo kileleni mwa msimamo wa ligi, huku kila timu ikihesabu matokeo yake kwa umakini mkubwa. Kwa mujibu wake, hakuna nafasi ya kufanya makosa katika hatua hii ya mwisho ya msimu.

Kamwe amesema Yanga inaendelea kupambana kuhakikisha inakusanya pointi zote zinazowezekana ili kufikia malengo yake ya msimu.

Amesisitiza kuwa wachezaji wanaelewa wajibu wao na wamejipanga kuhakikisha wanamaliza kazi waliyoianza kwa mafanikio.

Akiangazia mchezo unaofuata, Kamwe amesema macho yao sasa yanaelekezwa katika safari ya kwenda Arusha ambako watavaana na Fountain Gate FC, mechi ambayo ameielezea kuwa ngumu na inayohitaji maandalizi ya hali ya juu.

“Yanga inapiga hesabu za kupigania ubingwa na wenzetu wanaendelea kutufuatilia kwa karibu. Hivyo tunatakiwa kuhakikisha tunashinda mechi zetu zote zilizosalia,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa Fountain Gate FC ni timu nzuri yenye uwezo wa kutoa ushindani mkali, hivyo Yanga haitaidharau bali itaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa na dhamira ya kutafuta alama tatu muhimu katika mbio za kutwaa taji la ligi.

YANGA SCKWENYE PRESHA YA UBINGWA, MOALLIN ATOA MASHARTI MAZITO