Simba SC

PAMBA YAJIPANGA KUIVURUGA SIMBA KATIKA MBIO ZA UBINGWA

Vardo June 14, 2026 9:58 am

LIGI Kuu Bara inaendelea tena leo katika viwanja viwili tofauti, huku mechi kubwa inayosubiriwa ni Simba dhidi ya Pamba Jiji, kwenye Uwanja wa KMC, zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza. Mechi nyingine itazikutanisha Tanzania Prisons ikiikaribisha wabishi Dodoma Jiji.

Simba inasaka pointi tatu muhimu ili kuzidi kuufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, ikiachwa pointi mbili dhidi ya Yanga inayoongoza msimamo na pointi 60 baada ya mechi 25 kabla ya wa jana dhidi ya Mashujaa.

Ushindi wa Simba katika mechi hiyo, utazidi kuongeza presha ya ubingwa kwa watani hao, huku Pamba Jiji ikisaka ushindi ili kuendelea kujiweka katika sehemu salama ya kubaki Ligi Kuu Bara msimu ujao.

MARA YA MWISHO KUKUTANA

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa Kirumba, Pamba ililazimisha nyumbani sare ya bao 1-1 baada ya kusawazisha bao la wekundu hao waliotangulia kufunga kupitia Anicet Oura. Pao la Pamba lilifungwa na James Mwashinga.

Simba inafahamu ugumu wa mechi dhidi ya Pamba, ikikumbuka katika uwanja huo ilishinda kwa tabu dhidi ya Dodoma Jiji, bao la Ellie Mpanzu,lililotokana na penalti iliyokoswa na Clotous Chama na mechi kumalizika kwa Wanamsimbazi kushinda bao 1-0.

Simba haijaangusha alama yoyote katika mechi zake sita zilizopita na tangu itoke sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga, imeshinda mechi zote za Ligi Kuu Bara hadi sasa na inaendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo.

CHAMA NDANI

Habari njema kwa Simba ni kupona kwa kiungo wake fundi, Chama ambaye alipata majeraha katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji. Chama amekuwa muhimili mzuri katika kikosi hicho akichangia upatikanaji wa mabao akifunga nane na asisti sita.

Kupona kwake majeraha kunaweza kuwa tishio kwa Pamba ambayo itakuwa na kazi nzito kumtuliza kutokana na kiwango chake kwa sasa, lakini pembeni yake kutakuwa na Oura na Lebasse Gueye ambao ni hatari katika kikosi cha wekundu hao.

MSIKIE BARKER

Kocha wa Simba Steven Barker akizungumzia mchezo huo, alisema baada ya mapumziko mafupi wakati wa mechi za kimataifa za kalenda ya FIFA, wachezaji wake walipata mapumziko mazuri na sasa wako tayari kwa mechi dhidi ya Pamba.

“Tulipata muda mzuri wa kupumzika, wachezaji wetu hapo kabla walikuwa na uchovu mkubwa wa kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi. Sasa wako sawa tumefanya mazoezi ya kutosha, tunafahamu haitakuwa mechi rahisi. Hii ndio moja ya timu ambayo ilitupa mechi ngumu tulipokutana nayo kwao, hivyo tutakuwa makini tuweze kushinda,” alisema Barker.

REKODI ZA PAMBA JIJI

Pamba ilishatua jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni na wachezaji wake wote wako tayari na ikiwa imeshafanya mazoezi mara tatu tangu ituje mjini.

Pamba kwenye mechi zake tano za mwisho imeshinda moja tu ilipoichapa KMC kwa bao 1-0 ambao tayari wameshashuka daraja, ikipoteza tatu dhidi ya Prisons nyumbani, Azam ugenini na Singida Black Stars kisha ikatoa sare moja dhidi ya Dodoma.

Timu hiyo inayofundishwa na kocha Mkenya Francis Baraza, inashika nafasi ya saba kwenye msimamo na itahitaji ushindi ili kuendelea kusalia kwenye nafasi hiyo na kuepuka presha ya kushuka chini. Itaingia kwenye mchezo huo ikimtegemea mshambuliaji wake Mkenya Mathew Tegisi mwenye mabao saba.

MSIKIE BARAZA

Akizungumzia mechi hiyo, Baraza alisema wanatambua haitakuwa rahisi lakini wanataka kutafuta ushindi au sare ili wazidi kukaa sehemu salama katika msimamo wa ligi.

“Kucheza dhidi ya Simba haitakuwa mechi rahisi, hii ni timu kubwa, tumejiandaa kucheza nao kwa umakini zaidi. Tunahitaji ushindi au sare ili tusiende kukaa eneo baya kwenye ligi. Ligi ni ngumu hautakiwi kuendelea kuangusha pointi,” alisema Baraza.

PRISONS VS DODOMA

Mechi nyingine itakuwa jijini Mbeya, Uwanja wa Sokoine na wenyeji Tanzania Prisons itaikaribisha Dodoma Jiji.

Prisons itaingia kwenye mechi hiyo kwa hesabu kali ikitambua kwamba tayari KMC imeshashuka, ikisubiri kujua nani ataungana naye kwenda Championship, Wanajeshi hao wa Magereza wakiwa nafasi ya 15 juu ya KMC.

Wanajeshi hao walishusha presha kwenye mchezo wa mwisho waliposhinda ugenini dhidi ya Pamba kwa mabao 3-2. Kama itashinda itaruka hadi nafasi ya 14, ikitegemea na matokeo ya Mbeya City ambayo jana ilikuwa uwanjani dhidi ya Mtibwa Sugar.

RAJA CASABLANCA YAMKABIDHI NABI JUKUMU LA KUIFUFUA TIMU