Habari za michezo

RAJA CASABLANCA YAMKABIDHI NABI JUKUMU LA KUIFUFUA TIMU

Vardo June 14, 2026 9:48 am

KOCHA wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi ametangazwa kuwa mkufunzi mpya wa Raja Casablanca akichukua mikoba ya aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids, aliyetimuliwa wiki hii baada ya matokeo kutowafurahisha mabosi wa timu hiyo.

Nabi anarithi nafasi iliyoachwa na Fadlu ambaye msimu uliopita alikuwa katika benchi la Simba kabla ya kurejea Morocco alikowahi kupiga kazi.

Kocha huyo amesaini mkataba wa kuinoa Raja hadi Juni 2027 ukiwa na kipengele cha kuongeza muda kulingana na makubaliano.

Mtunisia huyo alijijengea heshima kubwa akiwa Yanga aliyoiacha baada ya kutwaa mataji sita yakiwemo mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili Kombe la Shirikisho (FA) na mawili Ngao ya Jamii, huku akiifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2023.

Baada ya hapo alitua AS FAR Rabat ya Morocco kabla ya kutimkia Kaizer Chiefs, Afrika Kusini ambako aliisaidia kutwaa Kombe la Nedbank.

Nabi anatua Raja wakati ikiwa kwenye kipindi cha kutafuta utulivu baada ya kupoteza mwendelezo wa matokeo na kushuka katika mbio za ubingwa.

Fadlu ameachana na miamba hiyo ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Morocco maarufu kama Botola Pro ikiwa na pointi 42, nyuma ya vinara Fes kwa tofauti ya pointi mbili.

MSIMU AVUNJA UKIMYA, AWEKA WAZI MUSTAKABALI NA SIMBA PAMBA YAJIPANGA KUIVURUGA SIMBA KATIKA MBIO ZA UBINGWA