Simba SC

MSIMU AVUNJA UKIMYA, AWEKA WAZI MUSTAKABALI NA SIMBA

Vardo June 14, 2026 9:43 am

KIUNGO wa Coastal Union, Bakari Msimu, ameweka wazi msimamo wake kuhusu taarifa zinazoendelea kumhusisha na usajili wa kujiunga na Simba SC, akisisitiza kuwa hadi sasa hajafanya uamuzi wowote rasmi kuhusu mustakabali wake wa kisoka.

Msimu amesema amekuwa akiziona taarifa mbalimbali zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii zikimtaja kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na klabu kadhaa kubwa nchini, ikiwemo Simba, lakini bado hajapokea taarifa rasmi kuhusu hatua inayofuata katika safari yake ya soka.

Nyota huyo ameeleza kuwa suala la hatma yake kwa sasa lipo mikononi mwa wasimamizi wake, ambao wataweka wazi mwelekeo wake mara baada ya kumalizika kwa msimu huu wa mashindano.

“Kwa sasa naona taarifa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, lakini nina imani mwisho wa msimu wasimamizi wangu watakuwa na majibu kamili kuhusu timu nitakayochezea,” alisema Msimu alipoulizwa kuhusu tetesi za kujiunga na Simba.

 

Licha ya kauli hiyo kutoweka wazi, taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa Simba imeonyesha nia ya dhati ya kumhitaji kiungo huyo kutokana na kiwango bora alichokionyesha akiwa na Coastal Union katika msimu huu.

Inaelezwa kuwa benchi la ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu Steve Barker limevutiwa na uwezo wa Msimu katika eneo la kiungo, jambo ambalo limeifanya klabu hiyo kuanza hatua za awali za kumshawishi kuhamia Msimbazi kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Taarifa hizo zinaongeza kuwa Simba imeandaa ofa nono kwa ajili ya mchezaji huyo, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa kusaini mkataba wa miaka miwili. Hata hivyo, hadi sasa hakuna tamko rasmi kutoka kwa Simba wala upande wa mchezaji kuhusu kukamilika kwa dili hilo

MASANZA AFUNGUKA KUHUSU BEKI YANGA, AWEKA WAZI KIPAUMBELE CHA SINGIDA BS RAJA CASABLANCA YAMKABIDHI NABI JUKUMU LA KUIFUFUA TIMU