Singida Big Stars FC

MASANZA AFUNGUKA KUHUSU BEKI YANGA, AWEKA WAZI KIPAUMBELE CHA SINGIDA BS

Vardo June 14, 2026 9:38 am

SINGIDA Black Stars imeweka wazi kuwa kwa sasa imeelekeza nguvu na umakini wake katika kuhakikisha inamaliza msimu kwa mafanikio, huku lengo kubwa likiwa ni kumaliza ndani ya nafasi nne za juu za Ligi Kuu Tanzania Bara ili kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa timu hiyo, Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Masanza, amesema bado wana mechi nne muhimu za ligi na kila mmoja ndani ya klabu anatambua umuhimu wa kupata matokeo mazuri katika michezo hiyo iliyobaki.

Masanza amesema kwa sasa akili na nguvu zao zote zimeelekezwa kwenye kutimiza malengo ya timu, akisisitiza kuwa nafasi ya nne ni muhimu kwao kutokana na nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumzia tetesi zinazoendelea kumhusisha beki wa Yanga, Patrick Mwenda, na kurejea Singida Black Stars msimu ujao, Masanza amesema ni mapema kuzungumzia suala hilo kwa kuwa dirisha la usajili bado halijafunguliwa na mchezaji huyo bado ana mkataba na klabu yake ya sasa.

Ameeleza kuwa Mwenda ni mmoja wa mabeki wazawa bora nchini na uwezo wake unafahamika wazi, lakini kwa sasa klabu hiyo haijajikita kwenye masuala ya usajili bali inawaza namna ya kumaliza msimu kwa mafanikio.

“Ni beki miongoni mwa mabeki wazawa bora tulionao Tanzania. Iwe anarejea au harejei, hilo haliondoi ubora wake. Masuala ya usajili bado yana muda wake,” amesema Masanza.

Ameongeza kuwa muda wa usajili ukifika, klabu itazungumzia kwa uwazi mipango yake ya kuimarisha kikosi, lakini kwa sasa kipaumbele ni kuhakikisha Singida Black Stars inafanikisha malengo yake ya kumaliza ligi katika nafasi nne za juu na kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

BEKI BORA DR CONGOATUA KWENYE MEZA YA SIMBA MSIMU AVUNJA UKIMYA, AWEKA WAZI MUSTAKABALI NA SIMBA