Simba SC

BEKI BORA DR CONGOATUA KWENYE MEZA YA SIMBA

Vardo June 14, 2026 9:35 am

HARAKATI za Simba SC kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao zimezidi kushika kasi, huku taarifa zikieleza kuwa mabosi wa klabu hiyo wameanza mazungumzo ya kumsajili beki wa kati wa TP Mazembe ya DR Congo, Madou Zon, anayeng’ara kwa kiwango bora msimu huu.

Madou amekuwa mmoja wa mabeki waliovutia zaidi katika Ligi Kuu ya DR Congo kutokana na uimara wake wa kujilinda, uwezo wa kusoma mchezo na uongozi wake ndani ya uwanja. Kiwango chake kizuri kimemfanya kutajwa miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya soka, Simba imeonyesha nia kubwa ya kuipata saini ya nyota huyo na tayari imeanza mazungumzo ya awali ili kuchunguza uwezekano wa kukamilisha dili hilo kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Inaelezwa kuwa awali Madou alikuwa karibu kujiunga na APR FC ya Rwanda baada ya kufikia makubaliano ya awali, lakini Simba imeingia kwa nguvu katika mbio hizo kwa kuwasilisha ofa inayodaiwa kuwa na thamani kubwa zaidi pamoja na mkataba wa miaka miwili.

Uongozi wa Simba unaamini kuwa ujio wa beki huyo utaongeza ushindani na uimara katika safu ya ulinzi, eneo ambalo linaonekana kupewa kipaumbele kikubwa kuelekea maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.

Mbali na ubora wake wa kujihami, Madou anatajwa kuwa na uzoefu mkubwa wa kucheza katika mechi za ushindani wa kimataifa akiwa na TP Mazembe, jambo ambalo linaonekana kuwavutia viongozi wa Simba wanaotaka kujenga kikosi chenye uwezo wa kufanya vizuri Afrika.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameridhishwa na wasifu wa beki huyo na amemuweka kwenye orodha ya wachezaji anaowahitaji.

“Endapo mazungumzo yatafanikiwa, Madou anaweza kuwa mmoja wa usajili mkubwa wa Simba katika dirisha hili la usajili”, amesema chanzo hicho

MSIMU WA MABINGWA WAFUNGULIWA MERIDIANBET KASINO MASANZA AFUNGUKA KUHUSU BEKI YANGA, AWEKA WAZI KIPAUMBELE CHA SINGIDA BS