Yanga SC

YANGA SCKWENYE PRESHA YA UBINGWA, MOALLIN ATOA MASHARTI MAZITO

Vardo June 14, 2026 3:35 pm

KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga SC, Abdihamid Moalin, amewataka wachezaji wake kuendelea kudumisha furaha, umakini na kutumia nguvu zao kwa akili kuelekea mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Moalin amesema kwa sasa hawana nafasi ya kupoteza umakini kutokana na kwamba zimebaki mechi nne muhimu na kila alama ina thamani kubwa katika mbio za ubingwa, akisisitiza kuwa kupoteza hata pointi moja kunaweza kuwaweka kwenye wakati mgumu.

Ameongeza kuwa licha ya ushindi walioupata dhidi ya Mashujaa FC, ambao uliwasaidia kuendelea kubaki kwenye ushindani, bado kikosi chake kinahitaji kujipanga zaidi kwa sababu mechi zilizobaki ni ngumu na zinahitaji nidhamu ya hali ya juu.

“Nashukuru tumemaliza salama mchezo wetu dhidi ya Mashujaa FC, hakuna majeraha na tumepata ushindi. Wachezaji wamepambana, lakini kwa sasa tunatakiwa kuwa makini zaidi na kutuliza akili kuelekea mechi zetu zijazo,” amesema Moalin.

Ameeleza kuwa mtihani ujao ni mchezo wa ugenini dhidi ya Fountain Gate FC, ambao wanatambua utakuwa mgumu, hivyo maandalizi ya kina yanahitajika ili kuhakikisha wanapata alama tatu muhimu.

Kikosi cha Yanga SC kimerudi Dar es Salaam kikitokea Kigoma, na kwa sasa kinaendelea na maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo kabla ya safari nyingine ya kuelekea Arusha kwa ajili ya mechi inayofuata, huku malengo yao yakiwa ni kumaliza msimu kwa mafanikio makubwa.

JENNIFER LOPEZ SINGLE MOTHER WA VIWANGO BAADA YA KUIFUNGA MASHUJAA, YANGA YAHAMISHIA VITA ARUSHA