Simba SC

POINTI 12 ZILIZOBAKI NI MATESO, AHMED AWAONYA SIMBA KUTOJISAHAU

Vardo June 15, 2026 5:54 pm

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema timu hiyo haina nafasi ya kustarehe katika hatua za mwisho za Ligi Kuu Tanzania Bara, akisisitiza kuwa pointi 12 zilizobaki kupiganiwa katika mechi nne zijazo ni muhimu na zinahitaji umakini mkubwa.

Ahmed amesema Simba imeingia katika kipindi kigumu cha msimu ambapo kila mchezo una uzito wake, hivyo wachezaji na benchi la ufundi wanapaswa kuendelea kushikamana na kutekeleza mipango waliyojiwekea ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya.

Ameeleza kuwa mechi zilizobaki si za kufurahia mapema wala kuhesabu pointi kabla ya kuzicheza, kwani kila mpinzani anapambana kwa malengo yake na ana uwezo wa kuleta ushindani mkubwa uwanjani.

“Mechi nne zimebaki, si za kufurahia. Ni ngumu sana. Kuna Mbeya City ambao tunaenda kucheza kwao na mara zote wanakuwa wapinzani wagumu. Pia kuna Singida Black Stars ambao nao wanahitaji maandalizi ya hali ya juu,” amesema Ahmed.

Amesema Simba inapaswa kuingia katika kila mchezo ikiwa na ari ya kupambana hadi dakika ya mwisho, akisisitiza kuwa hakuna nafasi ya kulegeza kasi katika mbio hizo za mwisho za ubingwa.

“Ni mechi nne za mateso, hakuna kustarehe. Muhimu ni kusimama katika mipango yetu na kuhakikisha tunashinda michezo yote iliyobaki,” ameongeza.

Ahmed pia alibainisha kuwa kupata ushindi katika hatua hii ya msimu si jambo rahisi, hata dhidi ya timu ambazo tayari zimepoteza nafasi ya kubaki ligi kuu, kwani nazo huingia uwanjani zikiwa na hamasa ya kujithibitisha.

Amesema hata kama Simba itakutana na KMC FC ambao tayari wameshuka daraja, bado watakuwa wapinzani wenye ushindani mkubwa, jambo linaloifanya Simba kuendelea kuwa makini katika kila dakika ya michezo iliyosalia.

SIMBA WAWEKA FURAHA YA USHINDI KANDO, WAANZA OPERESHENI MBEYA BELGIUM USO KWA USO NA EGYPT NANI KUIBUKA MSHINDI