Simba SC

SIMBA WAWEKA FURAHA YA USHINDI KANDO, WAANZA OPERESHENI MBEYA

Vardo June 15, 2026 5:47 pm

BEKI wa Simba, Ismael Oliver Touré, amesema siri ya mafanikio ya timu hiyo ni kutoweka muda mwingi kushangilia matokeo ya mechi zilizopita, badala yake kuanza mara moja maandalizi ya mchezo unaofuata.

Touré amesema mara baada ya kumalizika kwa dakika 90 za mchezo wao dhidi ya Pamba Jiji FC, wachezaji na benchi la ufundi hukutana kufanya tathmini ya mechi, kubaini makosa yaliyojitokeza na kuweka mikakati ya mchezo unaofuata.

Amesema ushindani mkubwa uliopo katika Ligi Kuu Tanzania Bara unawalazimu kuwa makini kila wakati kwani mashabiki wa Simba wanatarajia kuona timu ikipata matokeo chanya katika kila mchezo.

“Ushindani wa ligi ni mkubwa. Kila mchezaji hapa Simba anafahamu mashabiki wetu wanahitaji furaha kutoka kwetu, hivyo baada ya kila mechi tunaanza moja kwa moja maandalizi ya mchezo unaofuata,” amesema Touré.

Ameongeza kuwa kwa sasa wameweka pembeni matokeo ya mchezo dhidi ya Pamba Jiji na nguvu zote wamezielekeza katika pambano lijalo dhidi ya Mbeya City.

“Tumemalizana na Pamba Jiji na sasa akili na nguvu zetu tunaelekeza katika mchezo ujao dhidi ya Mbeya City. Hautakuwa mchezo rahisi, lakini tumejipanga kusaka alama tatu muhimu,” amesema.

Simba inaendelea kupambana katika mbio za ubingwa wa ligi, huku kila mchezo uliobaki ukiwa na umuhimu mkubwa katika kutimiza malengo ya msimu huu.

Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa na kibarua kizito Juni 17, 2026 watakaposhuka dimbani kuikabili Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, wakihitaji ushindi ili kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

MASHOSTI WALIOFICHA SIRI UJAUZITO WA WEMA SEPETU HADI KUJIFUNGUA POINTI 12 ZILIZOBAKI NI MATESO, AHMED AWAONYA SIMBA KUTOJISAHAU