Hesabu za Twiga Stars WAFCON 2026: Jinsi Tanzania Inavyoweza Kufuzu Robo Fainali
DAR ES SALAAM, Tanzania — Licha ya timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Burkina Faso katika mchezo wao wa pili wa Kundi B wa WAFCON 2026, matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali bado yapo mikononi mwao.
Hivi sasa, Tanzania inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu, ikilingana na Burkina Faso. Ivory Coast inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne, huku Afrika Kusini ikiburuta mkia na pointi yao moja. Msimamo huu unafanya kundi hili kuwa la wazi na kila timu kuwa na nafasi ya kutinga hatua inayofuata.
Mechi ya Maamuzi: Tanzania vs Ivory Coast
Mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi uliopangwa kuchezwa Agosti 4 dhidi ya Ivory Coast ndio utakaotoa hatima ya Twiga Stars, huku Burkina Faso wakichuana na Afrika Kusini.
Hizi hapa ndizo njia tatu na hesabu za Twiga Stars kufuzu robo fainali:
1. Ushindi Dhidi ya Ivory Coast (Njia ya Uhakika)
Ikiwa Twiga Stars itapata ushindani na kuondoka na pointi tatu, itafikisha pointi 6. Matokeo haya yatawapa uhakika wa kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye Kundi B na kufuzu moja kwa moja robo fainali.
-
Kumbuka: Iwapo Burkina Faso nayo itaifunga Afrika Kusini na kufikisha pointi 6, mshindi wa kundi ataamuliwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
2. Sare Dhidi ya Ivory Coast (Hesabu za Presha)
Tokeo la sare litawapa Twiga Stars pointi 4. Hapa mambo yatakuwa ya vuta-nikuvute kwani yatategemea matokeo ya mechi kati ya Burkina Faso na Afrika Kusini ili kujua nafasi watakayomaliza.
3. Kupoteza Mechi (Nafasi ya Best Loser)
Kipigo kitawafanya Twiga Stars kusalia na pointi 3. Hata hivyo, matumaini hayatakuwa yameisha kabisa; watapaswa kusubiri matokeo ya makundi mengine ili kuona kama wanaingia kwenye kipengele cha timu mbili bora zilizomaliza nafasi ya tatu (Best Losers) kufuzu robo fainali.