Hamisa Mobetto Avunja Ukimya Tetesi za Aziz Ki Kurejea Yanga SC
Huku homa ya usajili ikizidi kupamba moto kwenye soka la Tanzania, jina la kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Stephane Aziz Ki, limeibua gumzo zito kufuatia tetesi za uwezekano wa kurejea kwake klabuni hapo akitokea Wydad Athletic Club ya Morocco.
Tetesi hizo zimewafanya maelfu ya mashabiki wa Yanga kuelekeza nguvu zao kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya Hamisa Mobetto, mke wa Aziz Ki, ili kupata uhakika wa dili hilo linalotajwa kuwa miongoni mwa usajili mkubwa zaidi wa dirisha hili kama litakamilika.
Alichokisema Hamisa Mobetto
Akijibu maswali na jumbe lukuki anazopokea kutoka kwa mashabiki, Hamisa ameweka wazi kuwa anaziona taarifa hizo mtandaoni kama watu wengine, lakini hana mamlaka wala taarifa rasmi za kuthibitisha au kukanusha kurejea kwa nyota huyo Jangwani.
“Ninapata meseji nyingi sana za watu na kwenye komenti ninapoposti kitu kwa akaunti yangu Instagram wakiniuliza kama Aziz anarudi Yanga kucheza. Ukweli ni kwamba hata mimi naona hizo taarifa kama zinavyosambaa mitandaoni, lakini kwenye hilo sina jibu la kuwapa kwa sababu sina taarifa rasmi za kuthibitisha kama ni kweli au si kweli.”
Rekodi ya Aziz Ki na Hali Halisi ya Usajili
Aziz Ki alijijengea heshima kubwa ndani ya Yanga SC tangu alipotua mwaka 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast. Katika misimu miwili aliyotumikia jezi za njano na kijani, alikua tegemeo kubwa na kusaidia klabu hiyo:
- Kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
- Kutinga fainali ya kihistoria ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) msimu wa 2022/23.
Baada ya kumalizika kwa msimu wa 2024/25, nyota huyo wa Burkina Faso alijiunga na Wydad AC ya Morocco. Hadi sasa, hakuna tamko rasmi lililotolewa na uongozi wa Yanga SC wala kambi ya Aziz Ki, huku mashabiki wakiendelea kusubiri kuona kama utabiri wa tetesi hizi utageuka halisi kabla ya dirisha la usajili kufungwa.