Mapacha wa Kariakoo: Vita ya Simba na Yanga Uwanja wa Uhuru
Mapacha wa Kariakoo wanaendelea kutoa burudani ya aina yake mtaani kupitia tabia zao za kuigana, hasa kwenye maamuzi ya viwanja vya nyumbani na maandalizi ya mechi zao.
Kwenye mechi za matamasha yao ya mwanzo wa msimu, zote mbili zilitumia Uwanja wa Uhuru na kuondoka na matokeo mabaya baada ya kupokea vichapo—mmoja akikung’utwa na timu kutoka DRC Congo na mwingine na Msumbiji au Kenya. Baada ya vipigo hivyo, wote walihisi Uwanja wa Uhuru una “nuksi” na kuamua kuukimbia mara tu Ligi Kuu ilipoanza. Wakaelekea wilayani Kinondoni, mmoja akitumia Uwanja wa Manispaa ya Kinondoni (KMC Complex) na mwingine Uwanja wa Jeshi wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kwenye michezo ya kimataifa, sheria na kanuni ziliwabana kutohatarisha viwanja hivyo vya Kinondoni, ikawalazimu kupata mbadala. Mmoja alielekea Uwanja wa Azam Complex (Chamazi) na mwenzake akaenda Chang’ombe kwenye Uwanja wa Uhuru. Matokeo yakawa ya kishindo: yule wa Chang’ombe alimchakaza mpinzani wake kwa mabao 6-0, huku wa Chamazi akipata ushindi wa mabao 2-0, na wote wakafuzu hatua inayofuata.
Baada ya kuona mwenzake anapata ushindi mnono Chang’ombe, yule wa Chamazi ameanza mchakato wa kurejea taratibu Uwanja wa Uhuru. Ameamua kuanzia na mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya kimataifa katika uwanja huo ili kuandaa saikolojia ya mashabiki wake kabla ya kurejea rasmi kubanana na mtani wake wa jadi.