Timu ya Taifa ya Woodball Yaagwa Kwenda Kenya: Tanzania Kusaka Tiketi ya Dunia Taiwan
Timu ya Taifa ya Woodball Tanzania imeagwa rasmi leo kuelekea jijini Nairobi, Kenya, tayari kushiriki Mashindano ya 9 ya Kimataifa ya Woodball Championship yanayotarajiwa kurindima kuanzia Septemba 18 hadi 22, 2026, katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya.
Huu ni ushiriki wa kwanza kihistoria kwa Tanzania katika mashindano haya ya kimataifa. Kikosi hicho kimeingia kwenye kinyang’anyiro hicho kikilenga kufanya vizuri ili kupata fursa ya kufuzu Mashindano ya Dunia (World Cup) yatakayofanyika nchini Taiwan, Desemba 2026.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuvuta hisia za wengi huku yakishirikisha mataifa mbalimbali ikiwemo wenyeji Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Tanzania.
BMT Yataka Nidhamu na Uzalendo Kenya
Akizungumza Septemba 16, 2026, wakati wa hafla ya kuiaga timu hiyo na kuikabidhi Bendera ya Taifa, Afisa Michezo Mwandamizi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Charles Maguzu, aliwataka wachezaji kwenda kupambana kwa dhamira moja ya kuletea nchi heshima.
Maguzu alibainisha kuwa kikosi hicho kina sura halisi ya kitaifa kwani kinajumuisha wachezaji kutoka mikoa mbalimbali nchini badala ya kutegemea mkoa mmoja pekee.
“Timu hii ni ya taifa kwa sababu mchanganyiko wenu umehusisha mikoa mbalimbali kama Kigoma, Dodoma na mingineyo, sio Dar es Salaam tu. Hii inaonyesha utayari wetu kama nchi kwenda kupeperusha bendera yetu nchini Kenya,” alisema Maguzu.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuwa na nidhamu ya hali ya juu, uaminifu, uzalendo na kujitolea kwa kila mchezaji ili kuiga mfano wa timu nyingine za taifa zilizofanya vizuri kimataifa.
Wito kwa Wadau na Serikali Support Woodball
Mbali na hayo, Maguzu alitoa wito kwa Watanzania na wadau wa michezo kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuiwezesha timu za taifa kupata rasilimali fedha na vifaa bora vya michezo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Woodball Tanzania, Winjuka Makuza, alisema hatua hii ni kielelezo tosha cha kukua kwa mchezo huo nchini. Alishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha safari hiyo na kuahidi kupambana ili kurudi na ushindi.