Ludacris na Eudoxie
Habari za michezo

Ludacris na Mke Wake Eudoxie: Uhusiano Wao, Watoto na Misaada Afrika

Vardo September 18, 2026 8:39 am

Rapa maarufu kutoka nchini Marekani, Ludacris, ana uhusiano wa karibu sana na Afrika si tu kupitia muziki wake, bali pia kupitia ndoa yake na mrembo kutoka Gabon, Eudoxie Mbouguiengue. Wawili hawa wamedumu katika mahusiano kwa miaka 18 sasa, huku wakiendelea kuwa mfano wa kuigwa kupitia kazi zao za kijamii na malezi ya familia yao.

Ludacris, ambaye anakumbukwa vyema na mashabiki nchini Tanzania baada ya kutumbuiza katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam mwaka 2011, amekuwa akisifiwa na mkewe kama baba bora wa watoto wao.

Walivyokutana na Safari ya Ndoa Yao

Mkali huyo wa kibao cha “My Chick Bad” na nyota wa filamu za “Fast & Furious”, alikutana kwa mara ya kwanza na Eudoxie mwaka 2008 katika hafla ya kuchangisha fedha ya kila mwaka ya LudaDay jijini Atlanta. Hafla hiyo, ambayo ilianza mwaka 2005, ina lengo la kukusanya fedha za kusaidia watoto kupitia taasisi ya Ludacris Foundation.

Baada ya miaka sita ya uchumba na urafiki wa karibu, Ludacris alimvisha Eudoxie pete ya uchumba mnamo Desemba 26, 2014 wakiwa safarini ndani ya ndege. Masaa machache tu baadaye, walifunga ndoa ya siri na ya faragha nyumbani kwao, sherehe iliyohudhuriwa na ndugu wa karibu pekee.

Familia na Malezi ya Watoto wa Kike

Hadi sasa, wawili hao wamefanikiwa kupata watoto wawili wa kike: Cadence Gaelle (aliyezaliwa mwaka 2015) na Chance Oyali (aliyezaliwa mwaka 2021). Pia, Ludacris ana watoto wengine wawili wa kike, Karma na Cai, kutoka katika mahusiano yake ya awali.

Mapenzi yake kwa watoto wake wa kike yalimfanya kuanzisha mradi wa katuni kwenye mtandao wa Netflix uitwao “Karma’s World” mwaka 2021, uliohamasishwa na binti yake mkubwa, Karma. Kipindi hicho kinalenga kuwajengea watoto kujiamini, ubunifu na kujitambua.

Eudoxie ni Nani? na Misaada Yake Nchini Gabon

Eudoxie alizaliwa na kukulia Gabon kabla ya kuhamia Marekani akiwa kijana mdogo. Katika kitabu chake cha “Unspoken Angel: My Story Through Her Eyes” (2016), anaeleza changamoto alizopitia ikiwemo kutokujua Kiingereza alipowasili Marekani na ukatili aliyokumbana nawo akiwa mtoto.

Uzoefu huo ulimsukuma kuanzisha taasisi isiyo ya kiserikali ya Unspoken Angels mwaka 2013, inayowasaidia wasichana na wanawake waliopitia ukatili, hususan waliopo nchini Gabon. Mwaka 2020, Ludacris na watoto wao walitunukiwa uraia wa Gabon, hatua iliyozidisha viungo vyao na Afrika kupitia misaada mbalimbali wanayotuma mara kwa mara.

Timu ya Taifa ya Woodball Yaagwa Kwenda Kenya: Tanzania Kusaka Tiketi ya Dunia Taiwan Ngorongoro Heroes vs Ethiopia: Ngorongoro Heroes Yaikabili Ethiopia Kusaka Nusu Fainali CECAFA U-20