Ngorongoro Heroes vs Ethiopia: Ngorongoro Heroes Yaikabili Ethiopia Kusaka Nusu Fainali CECAFA U-20
Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, kesho Jumamosi inatarajia kushuka katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kukabiliana na Ethiopia katika mchezo muhimu wa pili wa Kundi A kuwania kufuzu Fainali za AFCON U-20.
Mchezo huo utakaopigwa majira ya saa 2:00 usiku unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku Ngorongoro Heroes ikisaka pointi tatu muhimu zitakazoihakikishia nafasi nzuri ya kutinga hatua ya nusu fainali.
Tanzania ilianza michuano hiyo kwa kishindo Septemba 15 baada ya kuichapa Rwanda mabao 3-0 katika mchezo wao wa kwanza. Ushindi huo uliifanya Ngorongoro Heroes kuongoza Kundi A ikiwa na pointi tatu na idadi nzuri ya mabao bila kuruhusu nyavu zao kuguswa. Kwa upande wa Ethiopia, matokeo haya yanawawekea presha kubwa na kuwalazimu kusaka matokeo mazuri ili kujiweka hai kwenye michuano hiyo.
Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Mario Rivera Campesino, ameeleza kuwa kikosi chake kipo tayari na kinaingia uwanjani kikiwa na kumbukumbu nzuri ya kiwango cha juu walichoonyesha dhidi ya Rwanda, hasa katika utengenezaji wa nafasi.
“Maandalizi yanaendelea vizuri na tunakwenda kwenye mchezo huu tukiwa na ushindani na ushindi wa kwanza. Hata hivyo, tunatakiwa kuboresha matumizi ya nafasi kwa sababu tunaendelea kutengeneza fursa nyingi za kufunga. Tukizitumia vizuri, tunaweza kupata ushindi wa mabao mengi zaidi kwenye michezo inayofuata,” amesema Campesino.
Mbali na mechi ya Tanzania na Ethiopia, mechi nyingine mbili zitapigwa siku hiyo ambapo Djibouti itakabiliana na Sudan saa 10:00 jioni, kisha Burundi itachuana na Kenya.