Kylian Mbappé Afunguka Uhusiano Wake na Wachezaji wa Real Madrid
Mshambuliaji nyota wa Real Madrid, Kylian Mbappé, ameweka wazi mtazamo wake kuhusu uhusiano kati ya wachezaji wa klabu hiyo nje na ndani ya uwanja, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kiutendaji ndio msingi mkuu wa mafanikio.
Mbappé amefananisha mazingira ya mpira wa miguu na wafanyakazi wa chombo cha habari au gazeti. Amesema kuwa si lazima kila mfanyakazi awe rafiki wa karibu wa mwenzake wanapokuwa nje ya kazi, lakini wanapokuwa kazini, sote tunafanya kazi pamoja kwa lengo moja la kuiletea klabu mafanikio na ushindi.
Ujumbe kwa Mashabiki wa Mitandao ya Kijamii
Akiwazungumzia mashabiki na wafuasi wa mpira katika kizazi hiki cha mitandao ya kijamii, Mbappé alibainisha kuwa watu wamekuwa wakiangalia mambo madogo sana na kuyatolea tafsiri zisizo sahihi.
“Mashabiki wa sasa wanaangalia hata kama mchezaji ametabasamu au kutosalimu mwenzake, kisha wanaanza kutengeneza drama na hisia ambazo hazipo.”
Ameongeza kuwa wachezaji wanafahamu vyema athari za mitandao ya kijamii, hivyo wanajitahidi kuwa makini sana ili kuzuia taswira yoyote inayoweza kuaminisha umma kuwa kuna migogoro au matatizo yasiyokuwepo ndani ya chumba cha kubadilishia nguo cha Real Madrid.