YANGA YAONGEZA MAKALI MBELE, HERSI AKAMILISHA DILI LA KUTIAMA
RAIS wa Yanga, Hersi Said, ameonekana kukamilisha moja ya kazi kubwa za usajili kuelekea msimu ujao baada ya kufanikiwa kuinasa saini ya mshambuliaji wa Police FC ya Kenya, Yves Kutiama, kwa mkataba wa miaka miwili.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa dili hilo lilifanikishwa mwishoni mwa wiki baada ya Hersi kuwepo nchini Kenya, ambako alishuhudia fainali ya Kombe la Mozzart Bet iliyozikutanisha Tusker FC na Police FC kwenye Uwanja wa Kwale, Juni 14, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Hersi alikutana na mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso na kufanya mazungumzo ya mwisho yaliyohitimishwa kwa kusainiwa kwa mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Yanga kuanzia msimu ujao.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa Yanga imekuwa ikimfuatilia Kutiama kwa muda kutokana na kiwango chake bora akiwa Police FC, ambapo uwezo wake wa kufunga na kuisumbua safu ya ulinzi ya wapinzani uliwavutia viongozi na benchi la ufundi la mabingwa hao wa Tanzania.
Mbali na Hersi, taarifa hizo zinaeleza kuwa kocha Benny Mwalala, ambaye amekuwa akihusishwa na Yanga, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya mshambuliaji huyo kabla ya uamuzi wa mwisho kufikiwa.
“Mwalala alipewa jukumu la kumfuatilia mchezaji huyo kwa karibu. Baada ya kuwasilisha ripoti yake, viongozi waliridhishwa na uwezo wake na hatimaye dili la kusainishwa kwake likakamilika. Mkataba wake ni wa miaka miwili,” kilisema chanzo hicho.
Ingawa Police FC ilipoteza fainali hiyo kwa mabao 2-1 dhidi ya Tusker FC, Kutiama aliendelea kuwa gumzo kutokana na kiwango chake, huku akitajwa kuwa miongoni mwa washambuliaji wenye uwezo mkubwa na matarajio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.