Simba SC

CHAMA AMEANDIKA HISTORIA, OKELLO BADO ANAJIFUNZA, CHIRWA

Vardo June 15, 2026 9:07 am

MSHAMBULIAJI wa Kagera Sugar, Obrey Chirwa, amesema bado ni mapema kumlinganisha kiungo wa Simba, Clatous Chama, na nyota wa Yanga, Allan Okello, akieleza kuwa wachezaji hao wako katika hatua tofauti za maendeleo ya soka.

Chirwa ambaye aliwahi kuchezea Yanga amesema Chama yupo katika kiwango cha juu zaidi kutokana na uzoefu wake mkubwa na mafanikio aliyoyapata ndani na nje ya Tanzania, jambo linalompa hadhi ya kipekee katika mchezo huo.

Kwa mujibu wa mshambuliaji huyo, Chama tayari ameandika historia yake katika soka la Tanzania na hata kwa taifa lake la Zambia kupitia mchango mkubwa alioutoa kwa miaka kadhaa aliyocheza hapa nchini.

“Okello ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na uwezo wa kufanya vizuri, lakini bado anahitaji muda zaidi wa kujifunza na kujijenga ili kufikia kiwango na mafanikio ambayo Chama ameyapata ndani ya soka la Tanzania,” amesema Chirwa.

Ameongeza kuwa kwa sasa Okello anatakiwa kuendelea kujifunza kutoka kwa wachezaji wenye uzoefu mkubwa waliothibitisha ubora wao kwa misimu kadhaa, akiwataja Chama, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua kuwa miongoni mwa nyota wanaoweza kumsaidia kukua zaidi.

Chirwa amesema haoni sababu ya kumpa Okello sifa nyingi kupita kiasi wakati akiwa amecheza kwa takribani miezi saba pekee katika soka la Tanzania, akisisitiza kuwa bado ana safari ndefu ya kufikia kiwango cha juu zaidi.

“Naona anatakiwa kuweka nguvu zaidi katika kazi yake na asiathiriwe na sifa nyingi kutoka kwa mashabiki. Bado ana nafasi kubwa ya kujifunza na kuendelea kuboresha kiwango chake,” amesema.

Amesisitiza kuwa mashabiki wana nafasi kubwa katika maendeleo ya wachezaji, kwani wanaweza kuwajenga au kuwaharibu kupitia kauli zao. Kutokana na hilo, amemtaka Okello kubaki mnyenyekevu na kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kudumisha na kuimarisha kiwango chake.

Akizungumzia msimu ujao, Chirwa amesema anaamini Chama ataendelea kuonyesha kiwango bora alichokizoea kwa mashabiki wa soka nchini, huku akimtaja Mudathir kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuendelea kung’ara kutokana na uwezo mkubwa waliouonyesha kwa misimu ya karibuni.

YANGA YAONGEZA MAKALI MBELE, HERSI AKAMILISHA DILI LA KUTIAMA KAULI NZITO YA MAGORI, SIMBA TUNAYOITAKA BADO HAIJAONEKANA