KAULI NZITO YA MAGORI, SIMBA TUNAYOITAKA BADO HAIJAONEKANA
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema kuwa licha ya timu hiyo kuendelea kufanya vizuri, bado viongozi hawajaridhishwa na kiwango kinachoonyeshwa na kikosi hicho kwa kuwa wanaamini kina uwezo wa kufanya zaidi ya kinachofanya kwa sasa.
Magori amesema mafanikio ambayo Simba imekuwa ikiyapata hayajawafanya viongozi kulewa sifa wala kuingiwa na presha ya matokeo, badala yake wanaendelea kufanya tathmini ya maendeleo ya timu ili kuhakikisha inafikia viwango vya juu walivyojiwekea.
Ameeleza kuwa matarajio ya viongozi na mashabiki wa Simba ni kuona timu ikicheza soka la kuvutia, lenye ushindani mkubwa na linaloweza kuipa mafanikio ya kudumu ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Magori, safari ya kufikia malengo hayo bado inaendelea, ndiyo maana hawataki kukimbilia kutoa hitimisho kuhusu ubora wa timu wakati bado kuna mambo kadhaa yanahitaji kuboreshwa ndani ya kikosi hicho.
“Sisi tunacheza ligi. Kuhusu ubingwa tutajua huko mbeleni. Mashabiki waendelee kuisapoti timu na kutuunga mkono katika juhudi za viongozi kuhakikisha tunafanikiwa kwenye kile tulichokilenga,” ameema Magori.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa uongozi wa Simba umeamua kubaki makini na kutazama safari ya msimu kwa mtazamo mpana badala ya kuangalia matokeo ya muda mfupi pekee.
Wakati ushindani wa Ligi Kuu ukiendelea kupamba moto, viongozi wa Simba wanaamini ushirikiano kati ya mashabiki, benchi la ufundi na wachezaji utakuwa silaha muhimu katika kuifikisha timu hiyo kwenye malengo makubwa ambayo imejiwekea msimu huu.