YANGA WATHIBITISHA KUCHEZA ZANZIBAR DHIDI YA AZAM FC
OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amethibitisha kuwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC utachezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Yanga wamechagua kuutumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani kutokana na Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuendelea kufanyiwa ukarabati, hali iliyowalazimu kutafuta venue mbadala kwa mechi hiyo muhimu.
Kamwe amesema uamuzi wa kuchagua New Amaan Complex umetokana na upatikanaji wa uwanja huo katika kipindi hiki ambacho ligi inakaribia kufikia tamati, huku viwanja vingi nchini vikiwa na ratiba mbalimbali za matumizi.
Ameeleza kuwa baada ya kumaliza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Azam FC utakaochezwa Mwanza, kikosi hicho kitarejea Dar es Salaam kabla ya kuelekea Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa ligi dhidi ya wapinzani hao.
“Baada ya mchezo wetu wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Azam FC ambao tutaucheza Mwanza, tutarejea Dar es Salaam na kisha kwenda Zanzibar kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC,” amesema Kamwe.
Mchezo huo unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi kutokana na umuhimu wake katika mbio za ubingwa, huku timu zote zikiendelea kupigania malengo yao kuelekea mwisho wa msimu.
Kwa upande wa Yanga, matumaini ni kuona wanatumia vyema uwanja wa New Amaan Complex ili kuendelea kujikusanyia pointi muhimu katika harakati za kutetea taji la ligi.