MPANZU NA GUEYE WAIBEBA SIMBA, PRESHA YAHAMIA YANGA
KAULI ya “kila mmoja ashinde mechi zake” inaendelea kutafsiriwa vitendo katika hatua za mwisho za Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Simba SC ikiendeleza presha kwenye mbio za ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Pamba Jiji FC.
Simba ilianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la mapema dakika ya nane kupitia kwa Elie Mpanzu, aliyemalizia vyema pasi ya Neo Maema na kuiandikia timu yake bao la kuongoza.
Hata hivyo, Pamba Jiji FC hawakukata tamaa na walirejea mchezoni dakika ya 18 baada ya Mathew Momanyi kufunga bao la kusawazisha na kufanya mchezo kuwa mgumu kwa wenyeji.
Katika kipindi cha pili, Simba iliendelea kushambulia kwa lengo la kutafuta ushindi muhimu. Jitihada zao zilizaa matunda dakika ya 65 pale Libasse Gueye alipofunga bao la pili ambalo lilithibitika kuwa la ushindi kwa Wekundu wa Msimbazi.
Ushindi huo umeifanya Simba kuendelea kuvuna alama tatu muhimu katika harakati zake za kuwania taji la ligi, huku ushindani kati yao na Yanga ukiendelea kuwa mkali kadri msimu unavyokaribia ukingoni.
Baada ya matokeo hayo, Simba imebakia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 61 baada ya kucheza mechi 26.
Kinara wa ligi ni Yanga SC mwenye alama 63, pia akiwa amecheza michezo 26, hali inayofanya mbio za ubingwa kuwa wazi zaidi huku kila timu ikihitaji kushinda mechi zake zilizobaki ili kutimiza malengo yake.