SIMBA YAWAPA JEURI VINGOZI, WADAI HAKUNA WA KUWAZUIA
UBORA unaoonyeshwa na Simba SC katika mechi zake za hivi karibuni umeendelea kuwapa kujiamini viongozi wa klabu hiyo, huku wakisisitiza kuwa kiwango cha soka kinachochezwa kwa sasa kinastahili pongezi kutoka kwa wadau wa mchezo huo.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Kocha Mkuu Steve Barker yameanza kuonekana wazi uwanjani, jambo ambalo limeifanya timu hiyo kuwa moja ya vikosi vinavyovutia zaidi kwa sasa.
Ahmed amesema Barker amefanikiwa kubadilisha mfumo wa uchezaji wa Simba na kuifanya timu kucheza soka la kisasa, lenye kasi, ubunifu na ushindani mkubwa, hali inayowafanya mashabiki na wadau wengi wa soka kufurahia wanapoitazama timu hiyo ikicheza.
Ameeleza kuwa nguvu ya Simba ya sasa haitokani na mchezaji mmoja pekee, bali ni matokeo ya ushirikiano wa kikosi kizima ambapo kila mchezaji anatimiza wajibu wake kwa kiwango cha juu ndani na nje ya uwanja.
Kwa mujibu wa Ahmed, uimara huo umeifanya Simba kuwa timu hatari kwa wapinzani wake, huku akiamini kuwa kiwango wanachokionyesha kwa sasa kinaendelea kutuma ujumbe mzito kwa timu nyingine zinazoshindana nao.
“Simba hii inatisha na ni hatari kwa mpinzani yeyote. Timu ikicheza mpira wa namna hii, nina uhakika kila mtu atapiga goti kwa ubora wa Simba ya sasa,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa bado wanaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kiwango hicho kinadumu hadi mwisho wa msimu.
Amesisitiza kuwa malengo yao ni kuendelea kupata matokeo mazuri na kuwapa furaha mashabiki wao ambao wamekuwa wakiisapoti timu katika kila hatua.