Michezo Bongo

MBEYA CITY YAPANIA KUIZAMISHA SIMBA, YATANGAZA VITA YA KUSALIA LIGI KUU

Vardo June 16, 2026 3:19 pm

KIKOSI cha Mbeya City kimeweka wazi dhamira yake ya kupambana hadi mwisho katika harakati za kujinasua na hatari ya kushuka daraja, huku kikielekeza nguvu zake kwenye mchezo muhimu dhidi ya Simba SC wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota, amesema timu hiyo imejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo huo, ikilenga kuvuna pointi tatu muhimu zitakazoongeza matumaini ya kuendelea kubaki ndani ya ligi msimu ujao.

Mwankota ameeleza kuwa kila mchezo uliosalia ni wa vita kwao kutokana na hali ya timu kuwa katika eneo la hatari la kushuka daraja, jambo ambalo limeongeza umakini na ari kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

Amekiri kuwa Simba ni timu imara yenye ubora mkubwa, lakini akasisitiza kuwa Mbeya City nayo ina sababu ya kupambana kwa nguvu zote kutokana na umuhimu wa pointi hizo katika safari yao ya kusalia Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa Mwankota, maandalizi maalum yamefanyika kwa siku kadhaa zilizopita, huku benchi la ufundi likifanya kazi ya kuwajenga wachezaji kimwili na kiakili ili kuhakikisha wanatumia vyema faida ya kucheza nyumbani mbele ya mashabiki wao.

“Wachezaji wetu, benchi la ufundi na menejimenti yote tumejipanga kwa ajili ya kupata ushindi katika mchezo huo. Tunaamini kwa ushirikiano wa mashabiki wetu tunaweza kufanikisha malengo yetu,” amesema Mwankota.

Mbali na mchezo dhidi ya Simba, Mbeya City pia imeelekeza macho kwenye mechi zake zilizobaki dhidi ya Dodoma Jiji, Pamba Jiji na TRA United.

Uongozi wa klabu hiyo unaamini kuwa matokeo mazuri katika michezo hiyo yanaweza kuwa tiketi muhimu ya kuisalia Ligi Kuu Tanzania Bara na kuepuka hatari ya kushuka daraja mwishoni mwa msimu.

YANGA YATUA ARUSHA KWA DHAMIRA YA KUVUNA POINTI TATU SIMBA YAWAPA JEURI VINGOZI, WADAI HAKUNA WA KUWAZUIA