HATUTADHARAU MTU, AHMED AWEKA WAZI MPANGO WA SIMBA
MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema kikosi hicho kinaendelea kuamini kuwa kina uwezo wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, huku wachezaji na benchi la ufundi wakiwa na ari kubwa ya kupigania taji hilo hadi mwisho wa msimu.
Ahmed alisema ndani ya Simba kwa sasa mawazo yote yameelekezwa katika mbio za ubingwa, akieleza kuwa kila mtu ndani ya klabu anatambua umuhimu wa mechi zilizobaki na wajibu wa kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
Amesisitiza kuwa Simba ina kikosi imara na chenye ubora wa kutosha wa kushindana katika ngazi ya juu, jambo linalowapa imani kubwa ya kufikia malengo waliyojiwekea mwanzoni mwa msimu.
“Ubingwa ndio kitu ambacho tunakiota na kukiwaza. Tunaamini timu ya kuchukua ubingwa tunayo,” alisema Ahmed Ally wakati akizungumzia safari ya timu hiyo kuelekea mwisho wa msimu.
Kwa mujibu wa Ahmed, Simba ni miongoni mwa timu zenye kikosi bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa na wanaocheza soka linalovutia mashabiki, hali inayowapa matumaini ya kuendelea kufanya vizuri.
Hata hivyo, ameeleza kuwa hakuna mchezo rahisi katika kipindi hiki cha mwisho cha msimu, kwani kila timu inapambana kutimiza malengo yake, jambo linalofanya ushindani kuwa mkubwa zaidi katika kila mechi.
Ahmed amezitaja Mtibwa Sugar, Singida Black Stars na KMC kuwa miongoni mwa wapinzani watakaohitaji umakini mkubwa, akisisitiza kuwa Simba haitadharau timu yoyote.
“Kila mechi kwetu ni muhimu. Hatutaki kudondosha alama hata moja,” alisema, akibainisha kuwa lengo lao ni kushinda mechi zote zilizobaki na kuendelea kuweka hai ndoto ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.