SIMBA YAJIPANGA KUVUNJA NDOTO ZA COASTAL UNION
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescetus Magori, amesema klabu hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha inafuzu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, huku akisisitiza kuwa hilo ni moja ya malengo makubwa yaliyowekwa na uongozi wa timu hiyo msimu huu.
Magori amesema Simba inaelewa umuhimu wa mchezo wa nusu fainali dhidi ya Coastal Union na kwamba maandalizi yote muhimu yamefanyika ili kuhakikisha timu inapata matokeo chanya na kusonga mbele katika michuano hiyo.
Kikosi cha Simba kiliondoka asubuhi ya leo kuelekea jijini Arusha kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo muhimu unaotarajiwa kuchezwa Juni 20, 2026, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Kiongozi huyo amesema wachezaji pamoja na benchi la ufundi wanafahamu matarajio makubwa ya klabu na mashabiki, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha timu inafikia lengo la kucheza fainali.
Magori amekiri kuwa Simba inatarajia kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Coastal Union, timu ambayo imeonyesha uwezo mkubwa katika michuano hiyo na kufanikiwa kufika hatua ya nusu fainali kwa juhudi zake.
“Hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu ni nusu fainali na wapinzani wetu ni wazuri. Lakini mipango yetu Simba inaitazama fainali. Hilo benchi la ufundi na wachezaji wanalitambua, na wao wanahitaji kufikia yale tunayotarajia kutoka kwao,” amesema Magori.
Kauli hiyo inaonyesha dhamira ya Simba ya kuendelea kupambana hadi mwisho katika Kombe la Shirikisho la CRDB, huku ikihitaji ushindi dhidi ya Coastal Union ili kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo muhimu nchini.